Jun 17, 2024 02:27 UTC
  • Saudi Arabia inatishia na kuchochea chuki dhidi ya mahujaji wanaotetea Palestina

Katika msimu huu wa ibada tukufu ya Hija, watawala wa Saudi Arabia wamejaribu kutisha, kuchochea chuki na kuwachafulia jina mahujaji wanaoonyesha mshikamano na watu wa Palestina huku kukiwa na malalamiko ya kimataifa kuhusu vita vya kikatili vinavyoendeshwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu Ukanda wa Gaza.

Maafisa wa Saudia wametumia maonyo na vitisho katika jaribio la kuzuia maandamano au nara zinazolaani vita vya mauaji ya halaiki ya Israel wakati wa kufanyika amali za siku tano za Hija, zilizoanza rasmi Ijumaa.

Ufalme wa Saudi Arabia unapotosha ukweli wa mambo kwa makusudi kwa kujaribu kufananisha malalamiko na maandamano halali ya watu wa Palestina wanaolaani jinai zinazofanywa dhidi yao na Wazayuni na vitendo vya ghasia katika maeneo matakatifu mjini Makka.

Huku akisisitiza suala hilo, Kanali Talal Al-Shalhoub, Msemaji wa Wizaya ya Mambo ya Ndani ya Saudia ameashiria kuwa utawala haramu wa Israel haupaswi kulaaniwa au kukosolewa katika maeneo hayo matakatifu ya Waislamu.

Wiki iliyopita, waziri wa Saudi Arabia anayesimamia masuala ya Mahujaji, pia alionya dhidi ya kuendeshwa shughuli zozote zinazounga mkono Palestina wakati wa Hija.

Tawfiq al-Rabiah amedai kwamba Hija ni kwa ajili ya ibada tu na si kutolewa kauli mbiu za kisiasa, na kuwa hivyo ndivyo wanavyotaka watawala wa ufalme huo ambao wameazimia kuhakikisha kwamba Hija inatumika kwa ajili ya kuonyesha unyenyekevu wa hali ya juu zaidi kwa Mwenyezi Mungu na utulivu wa kiroho tu.

Saudi Arabia imejaribu kujidhihirisha kama mtetezi wa kadhia ya Palestina lakini siasa na misimamo kama hiyo mara nyingi imeanika peupe unafiki wake kuhusu suala hilo.

Harakati ya Muqawama wa Palestina Hamas imezingatia sana ibada ya Hija ya mwaka huu kutokana na utawala wa Israel kuendeleza vita vya mauji ya umati dhidi ya Gaza ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 37,000.

Abu Obeida, Msemaji wa Brigedi ya Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Hamas amewaomba Mahujaji waiombee dua Gaza na taifa zima la Palestina, na kusisitiza kuwa msimu huu wa ibada tukufu ya Hija unaweza kutumika kama njia ya kupaza sauti ya kuujulisha ulimwengu machungu, mauaji ya umati, mateso na masaibu wanayoyapitia Wapalestina na jinai za kutisha zinazotekelezwa dhidi yao na utawala katili wa Israel.

Amesema, operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ilitekelezwa kwa ajili ya kutetea eneo la tatu takatifu zaidi katika Uislamu, na kuwa amali za Hija zinaweza kutumika kama fursa nzuri ya kuwakumbusha watu milioni mbili katika Umma wa Kiislamu kuhusu ukweli wa mapambano ya Wapalestina dhidi ya adui anayevunjia heshima eneo hilo takatifu la Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Saudi Arabia inaendelea kutekeleza kwa makusudi siasa za kuzima sauti ya wale wnaotetea na kuunga mkono taifa la Palestina na kabla ya hapo ilijaribu kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Israel kabla ya Oktoba 7, lakini ikalazimika kusitisha kwa muda juhudi zake hizo kutokana na kilio cha kimataifa kuhusu vita vya mauaji ya umati vya Israel huko Gaza.

Kwa sasa, ufalme huo unakandamiza sauti za wanaotetea Palestina katika ibada ya Hija ili kuiridhisha Israel.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, Saudi Arabia ilikuwa miongoni mwa nchi tano za Kiarabu ambazo maafisa wao wakuu wa kijeshi walifanya mazungumzo na wakuu wa kijeshi wa Israel na Marekani huko Bahrain Jumatatu iliyopita.

Hatua hizo zinaonyesha wazi kuwa licha ya Israel kuwaua kwa umati raia wa Palestina, lakini bado Saudi Arabia inataka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu.

Bila kujali vikwazo vilivyochochewa kisiasa ambavyo Saudi Arabia imewawekea mahujaji wanaoiunga mkono Palestina, kitendo hicho pekee kinapingana wazi na mafundisho ya Mtume Muhammad (saw).

Mtume wa Uislamu alitoa hotuba yake ya mwisho, inayojulikana kama 'Hotuba ya Kuaga', katika Mlima Arafat. Ni katika mlima huo ndipo Waislamu kutoka pembe zote za dunia hukusanyika katika siku ya pili ya ibada ya Hija kwa ajili ya kufanya ibada muhimu na kutafakari juu ya Mwenyezi Mungu mchana kutwa.

Katika hotuba hiyo, Mtume Muhammad alitoa wito wa kuwepo usawa na umoja baina ya Waislamu. Kwa siasa zake hizi mbovu, Saudi Arabia sio tu kwamba inashiriki katika mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza bali imefumbia macho wito uliotolewa na Mtume Mtukufu (saw) kuhusu udharura wa kujali maslahi ya Uislamu na Waislamu.

Tags