Jun 23, 2024 03:31 UTC
  • Jeshi la Yemen lashambulia manowari ya US kwa makombora

Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vimefanya shambulio jipya la makombora dhidi ya meli ya kivita ya Marekani katika Bahari Nyekundu.

Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema kuwa, meli hiyo kubwa ya kubebea ndege za kivita ya Marekani inayojulikana kama USS Eisenhower ililengwa kwa makombora ya balestiki na cruise ya kikosi cha wanamaji wa Yemen hapo jana katika maji ya Bahari Nyekundu.

Aidha vikosi vya Yemen hiyo jana vilishambulia meli ya mizigo ya Transworld Navigator iliyokuwa na bendera ya Liberia katika Bahari ya Arabia, kwa kutumia makombora ya balestiki.

Msemaji wa Jeshi la Yeman amesema mashambulio hayo ni muendelezo wa operesheni za kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, ambao wanaendelea kukabiliwa na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaosaidiwa na kuungwa mkono kikamilifu na Marekani.

Brigedia Jenerali Yahya Saree ameongeza kuwa, meli za Marekani na Uingereza zinazopita Bahari Nyekundu, Lango-Bahari la Bab al-Mandab, Ghuba ya Aden, na hata katika Bahari ya Arabia ni shabaha halali za vikosi vyake vya kijeshi.

Brigedia Jenerali Yahya Saree

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya ndege za kivita za Marekani na Uingereza kwa mara nyingine tena kushambulia kwa mabomu mkoa wa Hudeidah ulioko magharibi mwa Yemen. Nchi mbili hizo za Magharibi zimekuwa zikifanya mashambulizi makali katika maeneo mengine ya Yemen katika miezi kadhaa iliyopita.

Vikosi vya jeshi la Yemen vimeahidi kuendelea kuzishambulia meli za utawala huo au zile zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu katika Bahari Nyekundu hadi pale utawala wa Kizayuni utakaposimamisha mauaji ya umati na mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko Gaza.