Kiongozi wa Hamas asisitiza kudumisha utulivu huko Lebanon
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesisitiza juu ya kudumisha amani na usalama huko Lebanon.
Mipaka ya Lebanon na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu imeshuhudia makabiliano kati ya wanamuqawama wa Hizbullah na jeshi la utawala wa Kizayuni tangu utawala wa Kizayuni uanzishe vita dhidi ya Gaza; huku tahadhari kuhusu kupanuka mapigano kati yapande mbili zikiongezeka hivi karibuni.
Ismail Haniya amekutana na kuzungumza huko Qatar na Basil al Hassan Mkuu wa Kamati ya Mazungumzo ya Lebanon na Palestina na kusisitiza kuwa Hamas inataka kuona amani na utulivu ukidumishwa huko Lebanon.
Ismail Haniya pia amepongeza juhudi za serikali ya nchi hiyo katika ngazi zote na juhudi za Kamati ya Mazungumzo ya Lebanon na Palestina kwa ajili ya kuliunga mkono shirika la UNRWA na kuboresha mchango wake katika kipindi hiki.
Haniya pia amezitaja taarifa kuhusu kusitishwa mazungumzo ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza kuwa ni za uongo na kusema: Hamas itaendelea na juhudi zake ili kufikia makubaliano ya kumaliza vita kwa kuzingatia masharti yake.