Jul 18, 2024 05:48 UTC
  • Uingereza na Marekani zaendelea kushambulia Yemen kuunga mkono Wazayuni

Mapema leo Alkhamisi asubuhi, televisheni ya Al Mashirah ya Yemen imeripoti kuwa, ndege za madola vamizi ya Marekani na Uingereza zimefanya mashambulizi matatu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa al Hudaidah, magharibi mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Nalo shirika la habari la FARS limevinukuu vyombo vya habari vya Magharibi vikitangaza mapema leo asubuhi kwamba Marekani na Uingereza zimeendelea kufanya mashambulio katika ardhi ya Yemen. 

Ilikuwa ni Jumatatu usiku wakati Brigedia Jenerali yahya Sarii, Msemaji wa Majeshi ya Yemen alipotangaza kuwa, vikosi vya nchi hiyo vimefanya operesheni tatu za mafanikio katika Bahari ya Sham (Bahari Nyekundu) na Bahari ya Mediterania dhidi ya vyombo vya baharini vya madola ya kibeberu yanayounga mkono jinai zinazofanywa na Israel huko Palestina hasa Ghaza. 

Vikosi vya Yemen vilianzisha mapambano ya kuwasaidia ndugu zao Wapalestina kupitia kupiga marufuku chombo chochote cha baharini kutumia Bahari Nyekundu kuelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. 

Operesheni hizo za majeshi ya Yemen zimekuwa na mafanikio makubwa na zinaendelea kuisababishia Israel hasara zisizo na kifani. Hata wakati madola ya kibeberu kama Marekani na Uingereza yalipoamua kuanzisha upya mshambulizi dhidi ya Yemen kuwaunga mkono Wazayuni, zimeshindwa kufungua njia ya baharini kuelekea maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.

Si hayo tu, lakini pia jeshi la Yemen limeamua kushambulia vyombo vyote vya baharini vya Marekani na Uingereza katika Bahari ya Sham kutokana na madola hayo ya kibeberu kufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Yemen.