Wapalestina wapongeza uamuzi wa ICJ dhidi ya Israel
(last modified Sat, 20 Jul 2024 06:22:07 GMT )
Jul 20, 2024 06:22 UTC
  • Wapalestina wapongeza uamuzi wa ICJ dhidi ya Israel

Makundi ya kisiasa na kijamii ya Palestina yamepongeza uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kutazama ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa haramu na kinyume cha sheria.

Mahakama hiyo kuu ya Umoja wa Mataifa ilisema jana Ijumaa kuwa, upanuzi wa ujenzi wa vitongoji zaidi ya 230 vya walowezi katika ardhi hizo za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1967 ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, na kwamba ujenzi huo unaweza kuhesabiwa kuwa mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid).

ICJ imeutaka utawala haramu wa Israel uhitimishe uwepo wake 'haramu' katika maeneo hayo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu haraka iwezekanavyo.

Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina kama HAMAS, Harakati ya Mujahideen ya Palestina, Jihadul Islami na Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina (PFLP) zimepongeza uamuzi huo na kusema kuwa ni hatua chanya itakayopelekea kutengwa zaidi kimataifa utawala ghasibu wa Israel.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Riyad Maliki akizungumza na wanahabari mjini The Hague nchini Uholanzi amesema uamuzi wa ICJ ina umuhimu mkubwa kwa taifa la Palestina, haki na sheria za kimataifa.

Kadhalika  Riyad Mansour, Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema uamuzi huo wa jana Ijumaa wa ICJ ni hatua kubwa katika kuhitimisha ukaliaji wa mabavu wa miongo kadhaa wa ardhi za Wapalestina.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) 

Haya yanajiri huku Iran ikiutaka Umoja wa Mataifa kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel ili utii amri zote zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya vita vya mauaji ya kimbari vya utawala huo kwenye Ukanda wa Gaza.

Katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel, ICJ iliiamuru Israel kuchukua hatua zote ndani ya uwezo wake kuzuia mauaji ya kimbari huko Gaza, kuruhusu upatikanaji wa chakula bila vikwazo katika eneo la Palestina lililozingirwa, na kusitisha mara moja uvamizi wake wa kijeshi katika mji wa kusini wa Rafah. Utawala pandikizi wa Israel unaendelea kupuuza maagizo hayo yote ya ICJ.