Mzayuni: Baada ya Yemen kushambulia Tel-Aviv, anga ya "Israel" si salama tena
Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa jeshi la utawala wa Kizayuni amekiri kwamba jeshi la Israel limeshindwa vibaya katika kukabiliana na droni ya Yemen iliyopiga Tel Aviv na kusisitiza kuwa, kuanzia sasa anga yote ya "Israel" si salama tena; na eneo lolote la utawala wa Kizayuni linaweza kushambuliwa bila ya kuwa na nguvu za kujikinga.
Shirika la habari la Tasnim limenukuu uchambuzi wa duru mbalimbali za utawala wa Kizayuni kuhusu shambulizi la ndege isiyo na rubani ya Yemen (droni) iliyofanikiwa kupenya na kupiga katika kitovu cha utawala wa Kizayuni yaani Tel Aviv na kusema kuwa, hiyo ni fedheha na kufeli vibaya jeshi na vikosi vya ulinzi vya Israel.
Gazeti la kila siku la Kizayuni liitwalo Calcalist limemnukuu afisa huyo wa ngazi za juu wa jeshi la utawala wa Kizayuni bila ya kumtaja jina lake na kusema kuwa, operesheni ya ndege isiyo na rubani ya Yemen iliyopiga Tel Aviv inahesabiwa kuwa ni Oktoba 7 nyingine, wakati jeshi la Israel liliposhindwa kuzuia operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa iliyoongozwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Amesema, kufanikiwa Yemen kupiga katikati ya Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni ni uthibitisho wa kushindwa vibaya mno mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel na ni uthibitisho kuwa zile zama za anga salama na safi ya Israel zimeisha.
Huku hayo yakiripotiwa, Msemaji wa jeshi la Yemen amesema kuwa, Ghaza haijawahi kuwa peke yake bali ina washirika kutoka taifa kubwa ambalo ni tiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema hayo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijami wa X na kuongeza kuwa, awamu ya nne ya mashambulio ya kushtukiza ya Yemen dhidi ya utawala wa Kizayuni katika kuunga mkono Ghaza inazidi kushika kasi kwa namna ambayo baadaye itawapokonya Wazayuni na mamluki wao, hata fursa ya kufikiri.