Naim Qassem: Majibu ya Hizbullah yatauumiza vibaya utawala wa Kizayuni
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza uwa, majibu ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni ni jambo lisiloepukika na majibu hayo yatakuwa ya kuuumiza utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Sheikh Naim Qassem, amegusia jinsi utawala wa Kizayuni ulivyomuua shahidi Fuad Shukr, mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa Hizbullah ya Lebanon na kusema kuwa, kila pale mmoja wetu anapouawa shahidi, mauaji hayo huleta umoja na mshikamano mkubwa katika safu zetu.
Ameongeza kwa kusema: Kuuawa shahidi Kamanda Fuad Shukr kutakuwa na matunda makubwa. Sisi ndio wenye haki na tunapambana na mhimili wa shari kupitia utawala wa Kizayuni unaofanya jinai za kuangamiza kizazi, lakini sisi ndio washindi.
Siku ya Jumanne, utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia jengo moja la ghorofa ambalo ni makazi ya raia huko kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon na kuua shahidi watu kadhaa akiwemo Kamanda Fuad Shukr, na mshauri mmoja wa kijeshi wa Iran.
Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, Hizbullah ya Lebanon na harakati nyingine za muqawama zimeingia vitani kupambana na utawala dhalimu wa Kizayuni ikiwa ni kuwasaidia na kuwaunga mkono ndugu zao Wapalestina hasa wa Ghaza. Harakati hizo za muqawama wa Kiislamu zimekuwa zikitoa vipigo vikali kwa dola pandikizi la Israel, muda wote huo.