Hali ngumu za watoto wa Gaza na bwabwaja za Wamagharibi
Wakati Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu huko Palestina akitangaza kuwa mienendo isiyo ya kibinadamu ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina ni jinai ya kivita, duru za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu zinaendelea kunyamaza kimya mbele ya jinai hiyo na kukataa hata kuilaani kwa maneno tu.
Kwa mujibu wa Francesca Albanese, "kile kilichotokea kwa wafungwa wa Kipalestina katika Gereza la Sde Teiman (ambako wafungwa wa kiume wa Kipalestina wamelatiwa na askari wa Israel) kilifanyika kwa makusudi na kwa ushirikiano na wakuu wa magereza, na kila mwanadamu anashtushwa na ukimya wa vyombo vya habari vya Magharibi kuhusiana na jinai hiyo."
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu anaamini kuwa, maafisa wa serikali ya Israel wanafanya jinai kwa sababu wanajua kwamba, hawatafikishwa mahakamani. Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu mtenda jinai wa Israel, akiungwa mkono kikamilifu na Marekani, anafanya jinai za kila aina dhidi ya binadamu huko Gaza ili kujiokoa na kushindwa. Mojawapo nyenzo za mashinikizo yake kwa watu wa Gaza ili wakubali kushindwa, ni kulizingira eneo hilo na kutekeleza sera ya kuwatesa watu kwa njaa, hasa watoto wadogo, sambamba na mienendo ya kikatili dhidi ya wafungwa na mateka wa Kipalestina. Ali Sharifinia, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: “Kwa kutilia maanani ukweli kwamba uwezo wa watoto kustahamili njaa ni mdogo ikilinganishwa na watu wazima, utawala wa Kizayuni unaelekeza sehemu kubwa ya mashinikizo yake kwa watoto."
Ijapokuwa Wazayuni pia wameshindwa katika kutekeleza sera hiyo, lakini suala muhimu na la kuzingatiwa ni ukimya wa ulimwengu wa Magharibi na wale wanaodai kutetea haki za binadamu mbele ya ukatili huo. Utawala wa kibaguzi wa Israel pia unajaribu kuwapigisha magoti Wapalestina kwa kutumia fimbo ya njaa dhidi ya watoto na kuwatendea ukatili na unyama usio na mithili wafungwa wa Kipalestina.
Katika mahojiano yake na baadhi ya mashahidi na wafungwa walioachiliwa kutoka kwenye jela za utawala wa Kizayuni, gazeti la Washington Post limekiri kuwapo unyanyasaji wa kingono wa kimfumo na mbaya dhidi ya Wapalestina na limelitaja Kizuizi cha Sde Teiman kuwa ni "Guantanamo nyingine". Vilevile Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu amesema hakuna neno linaloweza kueleza ipasavyo uhalifu uliofanyika katika gereza hilo.
Ingawa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amelaani sera ya Israel ya kuwatesa kwa njaa watu wa Gaza, lakini kwa mtazamo wa Wapalestina, matamshi kama hayo ni bwabwaja za kionyesho tu zenye lengo la kupumbaza maoni ya umma katika nchi za Magharibi. Borrell amesema, kuua watu kwa njaa kwa makusudi ni uhalifu wa kivita, na kauli ya Bezalel Smotrich, waziri wa bishara Israel, kuhusu suala hilo, ni kielelezo cha kudharauliwa tena sheria za kimataifa na kanuni za kimsingi za ubinadamu...
Hata hivyo, kinachowashangaza walimwengu ni kwamba, kwa nini duru za Magharibi zinaendelea kukaa kimya mbele ya jinai za utawala wa Israel na kuruhusu uhalifu wa aina yoyote kutendeka huko Gaza na katika korokoro na jela za utawala huo wa kibaguzi?!!
Hakuna shaka kwamba, Wazayuni wanaendelea kufanya jinai hizo chini ya mwavuli wa himaya kamili ya Marekani na washirika wake wa Kimagharibi, na wana kinga kamili ya kuendelea kutenda jinai hizo. Pamoja na hayo, inatarajiwa kwamba, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa zitachukua hatua zaidi ya kulaani uhalifu huo na kukomesha jinai za Wazayuni dhidi ya watu wa Palestina.