Wazayuni wazidi kujawa na hofu na kiwewe cha kungojea ulipizaji kisasi wa Mhimili wa Muqawama
Aug 12, 2024 11:05 UTC
Utawala wa Kizayuni wa Israel umerefusha muda wa kuviweka katika hali ya tahadhari vikosi vya jeshi lake la anga kwa kuhofia madhara makubwa yatakayosababishwa na jibu la ulipizaji kisasi la Mhimil wa Muqawama kufuatia mauaji ya Ismail Haniya, aliyeuliwa shahidi na utawala huo wa kigaidi.
Shahidi Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na mmoja wa walinzi wake waliuawa shahidi tarehe 31 Julai kutokana na hujuma ya kigaidi iliyofanywa mjini Tehran.
Wasiwasi na mkanganyiko wa kiakili unaousokota utawala haramu wa Israel unazidi kuongezeka siku baada ya siku kwa kuhofia ukubwa wa jibu lisilo na shaka la Iran kwa mauaji ya Shahidi Ismail Haniya na la Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon kutokana na kuuliwa kamanda wake mkuu Shahidi Fuad Shukr.
Kwa mujibu wa IRNA, tovuti ya Walla ya utawala wa Kizayuni imeeleza kuhusiana na hilo kwamba kiwango cha hali ya hadhari ya intelijesnia ya kijeshi na jeshi la anga la Israel kimeongezwa kwa kuzingatia makadirio ya ukubwa wa jibu linalokaribia kutolewa na Iran.
Redio ya utawala wa Kizayuni imeashiria barabara zilivyobaki tupu na wasiwasi uliotanda kwenye uso wa kila Mzayuni na kuielezea hali hiyo kuwa ni sawa na ilivyokuwa wakati wa kipindi cha Corona.
Wasiwasi na hofu hiyo haijawapata wakazi pekee wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, bali imewakumba pia viongozi wa Kizayuni.
Yoav Gallant, waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni amesema katika mazungumzo yake na waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin kuhusu jibu la kulipiza kisasi la Iran kwa utawala huo ya kwamba: Iran inajiandaa kwa mashambulizi makubwa dhidi ya Israel; na makadirio ya shirika la ujasusi la Israel zinaonyesha kuwa, mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran kutokana na mauaji ya Haniya yatafanyika katika siku zijazo.
Kwa vile utawala wa Kizayuni hauwezi peke yake kuyahimili mashambulizi ya Tehran, viongozi wa utawala huo wanahitaji msaada wa Marekani kwa ajili ya kujilinda, sawa na ilivyokuwa katika shambulio la Iran la Aprili 14.../