Aug 22, 2024 03:06 UTC
  • 84% ya Misikiti ya Gaza imeharibiwa na mabomu ya Wazayuni

Asilimia 84 ya Misikiti katika Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu imeharibiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Press TV iliripoti hayo jana Jumatano, siku ambayo Wapalestina walijiunga na Waislamu wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Msikiti.

Kanali ya televisheni ya Press TV imeripoti kuwa, wakazi wa Gaza wameachwa bila sehemu yoyote ya kuabudia, kwani aghalabu ya Misikiti katika eneo hilo lililo chini ya mzingiro imeharibiwa kikamilifu au kwa kiasi fulani kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel.

Wizara ya Wakfu na Masuala ya Dini katika Ukanda wa Gaza imesema mashambulizi ya vikosi vya utawala katili wa Israel dhidi ya eneo hilo lililozingirwa yamebomoa na kuharibu maelfu ya Misikiti tokea Oktoba 7, 2023 hadi sasa.

Kadhalika mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Kizayuni yamepelekea kuuawa shahidi makumi ya wanazuoni, wahubiri, maimamu, na waadhini tangu Oktoba 7 hadi sasa. Aidha hujuma hizo za Israel dhidi ya Gaza zimeripotiwa kulenga ofisi za kamati za kukusanya zaka, madrasa za Qurani na makao makuu ya Benki ya Wakfu.

Wazayuni wasivyosaza hata maabadi Ukanda wa Gaza

Ikumbukwe kuwa, Mwaka 2003, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipendekeza katika mkutano wa 30 wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiislamu mjini Tehran kwamba, kutokana na nafasi muhimu ya Misikiti katika kuimarisha umoja na mshikamano wa Waislamu, iainishwe siku moja kuwa Siku ya Kimataifa ya Msikiti.

Baada ya pendekezo hilo, washiriki wa mkutano huo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamo OIC waliidhinisha kwamba, tarehe 21 Agosti ya kila mwaka ambayo ni siku ya kumbukumbu ya jinai iliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa Al-Aqsa, ipewe jina la "Siku ya Msikiti Duniani".

Tags