Sep 08, 2024 12:56 UTC
  • Hizbullah: Adui hana chaguo jingine ghairi ya kusitisha vita Gaza

Mjumbe wa Baraza Kuu la Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, adui ana njia moja pekee, ambayo ni kusimamisha hujuma na mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Vyombo vya habari vya Kiarabu vimemnukuu Sheikh Nabil Kaouk, Mjumbe wa Baraza Kuu la Hizbullah ya Lebanon akisema hayo leo Jumapili na kuongeza kuwa, "Muqawama unaweza kuleta milingano mipya ya nguvu katika eneo (la Asia Magharibi), na kwamba chaguo pekee la adui ni kusimamisha vita."

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Hizbullah amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unazidi kuwa dhaifu siku baada ya siku; katika hali ambayo nguvu ya Muqawama inazidi kukua na kustawi katika viwango vya kisiasa na kijeshi.

"Majibu ya Hizbullah kwa vitisho vya utawala wa Kizayuni yalithibitisha kwamba mrengo wa Muqawama hautasalimu amri mbele ya vitisho," ameongeza Sheikh Nabil Kaouk. Ameeleza bayana kuwa, utawala wa Kizayuni uko katika mkondo wa kuporomokoa na kushindwa huku makundi ya Muqawama ya Iraq, Palestina, Yemen na Lebanon yakielekea kwenye ushindi wa kistratijia na wa kihistoria.

Makombora ya Hizbullah

Mjumbe wa Baraza Kuu la Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, licha ya uungaji mkono wake wa kijeshi kutoka kwa Marekani na mashinikizo yake dhidi ya Wapalestina wa Gaza, lakini adui Mzayuni hana uwezo wa kutosha wa kulisambaratisha eneo la Ukanda wa Gaza, kwani Muqawama umedhamiria kupata ushindi.

Siku chache zilizopita, redio ya jeshi la Israel ilitangaza kuwa, Hizbullah ilifanya mashambulizi makubwa katika maeneo ya kaskazini mwa Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, kwa kuvurumisha makombora 1,307 mwezi Agosti.

Tags