Mamlaka za Ghaza zairejeshea Israel miili 88 ya Wapalestina isiyo na 'utambulisho' wowote
Sep 26, 2024 05:12 UTC
Mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Ghaza zimeurejeshea utawala wa Kizayuni wa Israel kontena lililobeba miili ya Wapalestina 88 ambayo haitambuliki kutokana na kutoambatanishwa na taarifa zozote kuhusu utambulisho wao.
Dr. Ismail Al-Thawabta, Mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza, amesema miili hiyo ilikabidhiwa na Israel huko kusini mwa ukanda huo ikiwa imetiwa kwenye kontena bila kufanyika uratibu wowote na Wapalestina au taasisi za kimataifa.
Dokta Thawabtah amefafanua kwa kusema: “imetolewa kwa njia ya kiburi na udhalilishaji ambayo inaonyesha dharau kwa utu wa Mashahidi. Hiki ni kitendo kisicho cha kibinadamu”.
Ameongezea kwa kusema, Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imeamua kuirudisha miili hiyo kwa Israel hadi taarifa na nyaraka zinazohusiana nayo zitakapotolewa".
Thawabtah amelaani kitendo hicho cha utawala wa Kizayuni akikielezea kuwa ni "jinai inayochukiza inayokiuka sheria za kimataifa na sheria za kibinadamu".
Amekumbusha kwa kusema: "hii haikuwa mara ya kwanza kwa upande wa Israel kufanya vitendo hivyo vya kinyama dhidi ya Mashahidi," na akayatolea wito mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Msalaba Mwekundu, "kuwajibika kwa kile kinachotokea."
Aidha amezitaka nchi za dunia ziushinikize utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe jinai zake za mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Utawala dhalimu wa Kizayuni ungali unaendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza ulivyoanzishwa Oktoba 7 mwaka jana licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja mapigano katika eneo hilo.
Hadi sasa Wapalestina wapatao 41,500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi na zaidi ya 96,000 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Ghaza.
Mashambulizi ya kinyama ya Israel yamewafanya karibu wakazi wote wa Ghaza kuwa wakimbizi kutokana na mzingiro unaoendelea ambao umesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa.
Ikumbukwe kuwa, utawala wa Kizayuni unakabiliwa na kesi ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa vitendo vya kinyama unavyoendeleza huko Ghaza.../
Tags