Oct 02, 2024 02:30 UTC
  • Qatar yataka mataifa ya Kiislamu kuungana kupambana na utawala wa Kizayuni

Waziri mshauri wa serikali ya Qatar katika masuala ya uhusiano wa kimataifa ameonya kuhusu hatari ya kuzuka vita vikubwa vya ukanda mzima wa Asia Magharibi na ametaka mataifa ya Kiislamu yaungane kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel unaofanya mauaji ya kizazi huko Palestina na Lebanon.

Bi Lolwah Al-Khater ametoa mwito huko kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuandika: Kama nchi za Kiislamu hazitoungana kupambana na utawala vamizi wa Kizayuni ambao unafanya jinai za kinyama katika eneo hili, basi miji yote ya nchi za Kiarabu itaathiriwa vibaya na jinai hizo na haitoishia Beirut na Ukanda wa Ghaza tu.

Matamshi ya waziri huyo wa Qatar yamekuja baada ya utawala mtenda jinai wa Israel kutangaza kuanzisha vita vya nchi kavu huko Lebanon na baadaye kuenea habari kwamba utawala wa Kizayuni umeogopa kuingia kwenye vita vya nchi kavu huko Lebanon.

Hayo yamethibitishwa na Muhammed Afif, Mkuu wa Kitengo cha Upashaji Habari cha Hizbullah ya Lebanon ambaye jana Jumanne aliiambia televisheni ya Al Jazeera kwamba madai yote ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuanzisha vita vya nchi kavu huko Lebanon ni ya uongo na wanajeshi wenye woga mkubwa wa Israel hawajatia mguu wao katika ardhi ya nchi hiyo.

Wakati anahojiwa na televisheni hiyo ya Qatar, Afif amesema, hadi wakati huo hakukuwa na uvamizi wowote wa nchi kavu wa wanajeshi wa Israel ndani ya ardhi ya Lebanon na kwamba wanamapambano wa Kiislamu wamejiandaa kikamilifu kukabiliana na uvamizi wa namna hiyo.

Tangu Jumatatu ya tarehe 23 Septemba 2024, utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya Lebanon hasa ya kusini.

Tags