Jumuiya ya Shanghai na upinzani dhidi ya vikwazo vya upande mmoja
(last modified 2024-10-19T02:33:18+00:00 )
Oct 19, 2024 02:33 UTC
  • Jumuiya ya Shanghai na upinzani dhidi ya vikwazo vya upande mmoja

Katika taarifa ya mwisho ya mkutano wa 23 huko Islamabad, mji mkuu wa Pakistan, viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai sambamba na kupinga vikwazo vya upande mmoja vya Magharibi dhidi ya nchi hizo, wamesema vikwazo hivyo vinaenda kinyume na sheria za kimataifa na kusisitiza kuwa kuwekwa vizuizi vya kibiashara kunavuruga maendeleo endelevu kimataifa.

Taarifa hiyo, imesisitiza kuwa nchi wanachama zinapinga hatua zote za upendeleo na vikwazo vya upande mmoja vya kibiashara ambavyo vinadhoofisha mfumo wa kibiashara wa pande kadhaa na kuvuruga maendeleo endelevu ya dunia. Hivyo nchi wanachama zinapanga kuimarisha mahusiano ya kisiasa na kiusalama, kibiashara, kiuchumi, kifedha, uwekezaji, kiutamaduni na kibinadamu ili kuunda dunia yenye amani, usalama, ustawi na usafi wa mazingira.

Kwa kuwa na zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote duniani na kuenea kijiografia kutoka kusini hadi mashariki mwa Asia na pia eneo la Eurasia, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, kama moja ya mashirika yenye nguvu kimataifa, ina uwezo mkubwa wa kubadilisha miundo ya kiuchumi na kijamii ili kutatua changamoto za kimataifa. Kwa mtazamo wa wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, ni jumuiya za Magharibi hususan za Marekani ndizo zinaweka vikwazo na sera za kibaguzi za upande mmoja, na hivyo kuvuruga utaratibu wa uchumi wa dunia, jambo ambalo linasababisha kuporomoka utaratibu wa miundo ya kijamii na kueneza umaskini duniani.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Shanghai

Kwa hivyo, wakuu wa serikali walioshiriki katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai huko Islamabad wamesisitiza juu ya kufanyika juhudi za pamoja kwa ajili ya kukabiliana na hatua za kibiashara zenye upendeleo na zilizo kinyume na sheria na kanuni za Shirika la Biashara Duniani, na pia kushughulikia suala la kuimarisha sheria za shirika hilo zinazoshajiisha uwazi, uadilifu na kupinga ubaguzi katika miamala ya kibiashara. Shirika la Biashara Dunianii. Pia wamesisitiza nia yao ya kuhakikisha maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika eneo la Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, na kutaka kutekelezwa mkakati wa maendeleo ya kiuchumi wa jumuiya hiyo hadi mwaka 2030 pamoja na mpango wa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi wanachama.

Kuwepo katika jumuiya hiyo nchi kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, China, Russia na India kunaipa nguvu kubwa katika mtazamo wa masuala kama vile fedha, nishati, usafirishaji na viwanda. Bila shaka, kujitenga na nchi za Magharibi na kupunguza uharibifu wao wa kiuchumi, kibiashara na kifedha kunahitaji kuundwa mifumo ya kifedha na kibiashara inayojitegemea tofauti kabisa na ya ulimwengu wa Magharibi. Hii ni kwa sababu nchi za Magharibi, hasa Marekani, hutumia miundo ya kifedha ya Magharibi kama vile Benki ya Dunia na SWIFT kutekeleza sera zao za mashinikizo na vikwazo dhidi ya nchi huru. Kwa hivyo, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ina uwezo wa kujenga nguvu ya kifedha na kiuchumi ya kusini mwa dunia na hivyo kuunda ulimwengu wenye ustawi, usalama na amani. Kwa kuzingatia kwamba nchi nyingi wanachama wa Shanghai ziko chini ya vikwazo au mashinikizo ya kiuchumi ya nchi za Magharibi, bila shaka zina motisha na azma inayohitajika kwa ajili ya kutimiza lengo na mpango huo.