Ndege za kivita za US na UK zashambulia miji ya Yemen
Marekani na Uingereza zimefanya mashambulizi kadhaa ya anga dhidi ya maeneo tofauti katika mkoa wa Sana'a na maeneo mengine ya Yemen, ili eti kukabiliana na operesheni za nchi hiyo ya Kiarabu dhidi ya Israel.
Mtandao wa televisheni ya al-Masirah ya Yemen ukinukuu duru za kiusalama ikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina uliripoti kwamba, mashambulio manne ya anga yamelenga eneo la Jarban katika wilaya ya Sanhan katika mji mkuu wa Sana'a alfajiri ya leo Jumapili.
Habari zinasema kuwa, ndege za kijeshi za Marekani na Uingereza pia zimelenga eneo la Haffa katika jimbo hilo hilo. Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa mara moja juu ya hujuma hizo mpya za kichokozi.
Kadhalika mashambulizi mawili ya anga yamelenga wilaya ya Harf Sufyan katika mkoa wa kaskazini-magharibi mwa Yemen wa 'Amran. Hakuna ripoti za majeruhi au uharibifu zilizotolewa kufikia sasa.
Hujuma hizi mpya za US na UK zinajiri katika hali ambayo, wananchi wa Yemen wametangaza uungaji mkono wao wa wazi kwa mapambano ya Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel tangu utawala huo ghasibu ulipoanzisha vita vya kutisha dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba mwaka jana na kuua Wapalestina wasiopungua 43,469 hadi sasa.
Jeshi la Yemen, katika kutii matakwa ya wananchi, limesema kuwa halitasimamisha mashambulizi yake dhidi ya Marekani na Israel na waitifaki wao hadi pale mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza yatakapokomeshwa.