Jul 24, 2016 07:49 UTC
  • 30 wauwa na kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi Baghdad, Iraq

Kwa akali watu 10 wamethibitishwa kupoteza maisha na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika shambulizi la bomu lililotokea mapema leo katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Polisi ya Iraq imesema kuwa, mshambuliaji wa kujitolea muhanga alijiripua katika kituo cha upekuzi kilichoko katika wilaya ya Kadhimiya, kaskazini mwa Baghdad na kusababisha maafa na majeraha hayo. Habari zaidi zinasema kuwa, walioawa katika hujuma hiyo ya kigaidi ni raia wanane na maafisa usalama wawili na kwamba zaidi ya watu 20 wamejeruhiwa. Mashambulizi ya aina hii sio mapya kufanyika katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Wahanga wa mashambulizi ya Karrad, Baghdad, Julai 3

 

Hujuma ya kigaidi katika mtaa wa Karrad mjini Baghdad Julai 3 ilikuwa mbaya zaidi nchini Iraq tokea uvamizi wa Marekani nchini humo miaka 13 iliyopita, ambapo watu zaidi ya 300 waliuawa. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq Mohammed Salem al-Ghabban alitangaza kujiuzulu kufuatia hujuma hiyo. Aidha Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi amewafuta kazi maafisa wa ngazi za juu wanaosimamia usalama katika mji mkuu Baghdad kufuatia hujuma ya kigaidi.

Itakumbukwa kuwa, kwa akali watu 58 waliuawa na wengine zaidi ya 90 walijeruhiwa katika mashambulizi matatu ya mabomu yaliyoutikisa mji mkuu wa Iraq, Baghdad Mei 17.

Tags