Hizbullah yashambulia maeneo ya kistratijia ya utawala wa Kizayuni wa Israel
(last modified Sun, 17 Nov 2024 02:27:16 GMT )
Nov 17, 2024 02:27 UTC
  • Hizbullah yashambulia maeneo ya kistratijia ya utawala wa Kizayuni wa Israel

Kituo cha Taarifa za Vita cha Hizbullah ya Lebanon kimetangaza kuwa wapiganaji wa harakati hiyo wamefanya mashambulizi ya makombora katika maeneo kadhaa ya kistratijia ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hizbullah ya Lebanon imetangaza mapema jana kwamba, imelenga kituo cha jeshi la wanamaji wa Israel cha "Stila Maris" kilichoko kaskazini magharibi mwa bandari ya Haifa kama kituo cha kistratijia cha ufuatiliaji na udhibiti wa jeshi la utawala wa Kizayuni katika pwani ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Jeshi la Israel limekiri kuw, leo asubuhi bandari ya Haifa na eneo la Al-Jalil huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu yalishambuliwa kwa makombora mazito yasiyopungua 35 kutoka kusini mwa Lebanon.

Kituo cha Taarifa za Vita cha Hizbullah ya Lebanon pia kimetangaza kuwa wapiganaji wa harakati hiyo wameshambulia kwa makombora makao makuu ya Brigedi ya Golani kaskazini mwa mji unaokaliwa kwa mabavu wa Acre na makao makuu ya Brigedi ya Magharibi ya jeshi Israel huko Yara Barracks, kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Wakati huo huo, takwinu zinaonyesha kuwa, idadi ya walowezi wa Kizayuni wanaokimbilia nje ya ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel inaendelea kuvunja rekodi siku baada ya siku kutokana na vipigo inavyopata Israel kutoka kwa wanamapambano wa Lebanon na Palestina.

Kwa mfano katika ripoti yake ya karibuni kabisa, gazeti la Kizayuni la Haaretz limeripoti kwamba zaidi ya walowezi 10,000 wamekimbilia Canada kutoka katika ardhi za Palestina walizokuwa wanazikalia kwa mabavu kutokana na vipigo vikali wanavyopata kutoka kwa wanamapambano wa kambi ya Muqawama.