Kiongozi wa Ansarullah awakosoa walimwengu kwa kupuuza maafa ya Wapalestina
(last modified Fri, 10 Jan 2025 07:01:24 GMT )
Jan 10, 2025 07:01 UTC
  • Kiongozi wa Ansarullah awakosoa walimwengu kwa kupuuza maafa ya Wapalestina

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amekosoa kimya na kutojali nchi tofauti za dunia hali ya njaa na mauaji ya kimbari yanayowakabili Wapalestina.

Sayyid Abdul Malik al-Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, jinai ya kuwaua kwa njaa wananchi wa Palestina haiishii tu kwa adui Mzayuni na kwamba serikali zote zuilizopuuza hali hiyo zinahusika katika jinai hiyo na vitendo vya kupora shehena za bidhaa za chakula zinazoelekea Ukanda wa Gaza.

Aidha amesema, adui Mzayuni ameunda makundi ya wahaini na mamluki ili kupora misaada inayotumwa katika Ukanda wa Gaza.

Sayyid al-Houthi amesisitiza kuwa, jeshi la Israel linapora moja kwa moja misaada inayoingia katika Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa, adui Mzayuni kwa makusudi ametengeneza hali mbaya katika Ukanda wa Gaza na amelenga kwa uratibu maalumu miundombinu yote ya afya.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameeleza kuwa, jinai iliyozofanywa na adui Israel katika Hospitali ya Kamal al-Adwan katika Ukanda wa Gaza ni ukiukaji wa wazi na ni moja ya jinai kubwa zaidi zilizofanywa katika karne hii.

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa Kizayuni ulianzisha vita vya kutisha dhidi ya Ukanda wa Gaza, ambapo asilimia 70 ya nyumba na miundombinu ya ukanda huo imeharibiwa vibaya, mzingiro mbaya na mgogoro mkubwa wa kibinadamu, pamoja na njaa isiyo na kifani vimegharimu maisha ya wakazi wa eneo hilo.