Wanamichezo 708 wameuawa shahidi tangu kuanza vita vya Gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyombo vya Habari vya Michezo vya Palestina ametangaza kuwa, wanamichezo 708 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika vita vya Gaza.
Mustafa Sayam, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vyombo vya Habari vya Michezo vya Palestina amesema hayo leo na kueleza kwamba, vita vya mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ghaza vimesababisha kuuawa shahidi wanamichezo 708 wa Kipalestina na kuharibiwa vituo 273 vya michezo katika Ukanda wa Gaza.
Sayam amesisitiza kuwa Israel imeharibu kabisa au kwa kiasi vituo 273 vya michezo katika vita vya Gaza, jambo ambalo litakuwa na madhara makubwa kwa maelfu ya wanamichezo wa Kipalestina.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hivi karibuni pia Shirikisho la Soka la Palestina lilitangaza kuwa, mamia ya wanamichezo wameuawa shahidi tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha hujuma na mashambulio ya kinyama dhidi ya Gaza Oktoba 2023.
Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya kundi la muqawama la Hamas la Palestina kufanya operesheni ya kihistoria dhidi ya utawala huo ikiwa ni kulipiza kisasi jinai za miongo kadhaa za Wazayuni dhidi ya Wapalestina.
Takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu kuanza hujuma kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni huko Gaza imepindukia 46,000.