Utawala wa Israel umetekeleza uharibifu mkubwa na wa makusudi Gaza
(last modified Wed, 22 Jan 2025 02:46:02 GMT )
Jan 22, 2025 02:46 UTC
  • Utawala wa Israel umetekeleza uharibifu mkubwa na wa makusudi Gaza

Katika kipindi hiki cha kutekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na kuondoka kwa vikosi vya utawala wa Kizayuni wa Israel, maelfu ya Wapalestina wanapaswa kurejea katika. Hata hivyo hakuna nyumba za kurejea kwani Gaza imebaki na magofu tu.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema kuwa Gaza inahitaji mabilioni ya dola kwa ajili ya ujenzi na kuondoa mabomu yaliyosalia. Amesema: "Tuko tayari kusaidia mchakato wa kusambaza misaada ya kibinadamu kwa watu wa Palestina huko Gaza. Tunatarajia kuweza kuingiza mamilia ya malori ya kila siku katika eneo hilo."

Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa sehemu kubwa ya miundombinu ya Gaza imeharibiwa, na Umoja wa Mataifa unafanya juhudi kubwa kwa ajili ya ujenzi wa upya.

Hali ya Gaza ni mbaya. Zaidi ya asilimia kubwa ya miundombinu imeharibiwa. Utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mashambulizi kwa malengo ya kuharibu miundombinu hiyo kwa njia ambayo Gaza isiwe tena mahali pa kuishi.

Lengo la uharibifu huo ni kutoa fursa kwa utawala ghasibu wa Israel kupanua udhibiti wake, kunyakua ardhi zaidi, na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni Gaza.

Hospitali, shule, na nyumba zimeharibiwa kabisa, na katika baadhi ya maeneo, mitaa yote imebomolewa kikamilifu na kilichosalia ni magofu. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya asilimia 90 ya majengo ya makazi ya Gaza yameharibiwa.

Taarifa za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa nyumba 160,000 za makazi zimeharibiwa kabisa, na nyumba zingine 276,000 zimepata uharibifu mkubwa.

Aidha, mashamba ya kilimo yameharibiwa na kubadilishwa kuwa milima ya mchanga na vifusi kupitia mabuldoza, vifaru na mizinga ya Israeli.

Pamoja na uharibifu wote, sasa kwa kuanza kwa kusitisha mapigano, wakazi wa Gaza wanarejea nyumbani. Wengi wao si tu kwamba wamepoteza nyumba na maisha yao, bali pia wamepoteza wapendwa wao. Shirika la Habari la Ufaransa lilimnukuu mmoja wa wakimbizi akisema: "Maisha yetu yameharibiwa. Itachukua angalau miaka ishirini kujenga tena maisha ya kawaida."

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa vita vya Gaza vimeacha zaidi ya tani milioni 50 za vifusi, ambavyo kuondolewa kikamilifu vifusi hivyo kutachukua zaidi ya miaka 15. Pia, kazi ya kuondoa vifusi inakabiliwa na changamoto kubwa kwa kuwa vina mabomu mengi ambayo hayajalipuka, vifaa hatari, na hata mabaki ya miili ya binadamu.

Kwa upande mwingine, uhaba wa chakula na vifaa vya matibabu unaendelea kuwa tatizo kubwa. Shirika la Afya Duniani limeelezea wasiwasi wake juu ya uharibifu kamili wa sekta ya afya na kusema kuwa ukanda wa Gaza unahitaji uwekezaji mkubwa kwa ajili ya ujenzi wa sekta hiyo. Kwa mujibu wa makadirio ya shirika hilo, Gaza inahitaji angalau dola bilioni 10 kwa ajili ya kujenga upya miundombinu ya afya. Katika sekta ya chakula na dawa, hali ni mbaya zaidi. Watoto zaidi ya 3,500 wanakabiliwa na vifo kutokana na utapiamlo, na hakuna dawa kwa ajili ya wagonjwa 350,000 wenye magonjwa sugu, hali inayohatarisha maisha ya watu wengi.

Watoto wa Gaza, wahanga wakuu wa jinai za Israel Gaza

Ukosefu huu umepelekea kuenea kwa magonjwa hatari, hasa miongoni mwa wakimbizi. Kwa sasa, malori ya misaada yanaelekea Gaza, lakini mahitaji ya chakula na dawa ni makubwa sana. Hakuna mfumo wa afya unaofanya kazi, na hakuna vituo vya matibabu pamoja wala madaktari .

Saed Hassouna, mwanahabari kutoka Gaza, anasema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Gaza wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula, na zaidi ya watu 300,000 wanateseka na njaa kali. Watu zaidi ya 50 walifariki mwaka uliopita kutokana na njaa.

Baada ya miezi 15 ya vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza, wakazi hao bado wanasimama imara na kwa matumaini wakirejea katika ardhi yao. Licha ya matatizo na uharibifu mkubwa, wanaanza safari ya kuijenga tena Gaza.