Trump ang'ang'ania mpango wake wa kutaka Wapalestina wahamishwe Ghaza, amwalika Netanyahu
Jan 29, 2025 03:28 UTC
Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kung'ang'ania pendekezo lake la kuhamishwa Wapalestina wote katika Ukanda wa Ghaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Trump amerudia tena kuzungumzia suala hilo lililopingwa na kulaaniwa vikali kimataifa, akiwa mbele ya waandishi wa habari Ikulu ya White kwa kusema: "ningependa niwafanye waishi katika eneo ambalo wanaweza kuishi bila usumbufu na mapinduzi na machafuko" .
Rais huyo wa Marekani aliibua suala hilo kwa mara ya kwanza siku ya Jumamosi na kupendekeza Jordan na Misri zichukue idadi nyingine kubwa zaidi ya Wapalestina wa Ghaza.
Siku ya Jumapili, nchi zote hizo mbili zilisisitizia msimamo wao wa awali wa kukataa kuwapatia makazi mengine Wapalestina mara baada ya Trump kutoa wito wa kufanywa kile alichokiita "kusafishea" eneo la Ghaza.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari Trump amesema, ameshazungumza pia na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi kuhusu suala hilo.
Amedai kwa kusema: "unapoutazama Ukanda wa Ghaza, umekuwa jehanamu kwa miaka mingi sana…zimekuwepo staarabu mbalimbali kwenye ukanda huo. Hayakuanzia hapa. Yalianza hapo kabla maelfu ya miaka, na kila mara kumekuwa na machafuko yanayohusiana nayo. Ungeliweza kuwapatia watu waishi katika maeneo ambayo ni salama zaidi na labda bora zaidi na pengine ya raha zaidi ".
Aidha, rais huyo wa Marekani amesema, atajadili suala hilo na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu, ambaye amesema anatarajiwa kuzuru Marekani "karibuni hivi".
Pendekezo la Trump, lililowaghadhibisha na kuwashangaza wengi limetolewa wiki moja baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa huko Ghaza mnamo Januari 19, ili kukomesha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel, ambayo yameteketeza roho za zaidi ya Wapalestina 47,300, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi wengine zaidi ya 111,000, tangu Oktoba 7, 2023.../
Tags