Ben-Gvir: Israel imegeuzwa kuwa 'kioja' Mashariki ya Kati
Aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani wa Israel, Itamar Ben-Gvir amesema utawala huo wa Kizayuni umekuwa kioja na kichekesho katika eneo la Asia Magharibi.
Licha ya kukiri kuwa Israel inazidi kuporomoka katika eneo hili, lakini mwanasiasa huyo mwenye siasa kali za mrengo wa kulia ametoa wito kwa wakazi wa Gaza kuhamishwa mara moja na kupelekewa katika nchi jirani.
Ben Gvir, ambaye alijiuzulu kutoka kwa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu kutokana na makubaliano ya kusitisha mapigano na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, amesema kuhamishwa kwa lazima wakazi wa Gaza kunapaswa kuanza haraka iwezekanavyo.
Amesema wakati Rais wa Marekani Donald Trump anaamini kuwa bado kuna wakati, lakini maslahi ya Israel hayawezi kuendelea kuvumilia kuahirishwa kwa hatua hiyo ya kufurushwa wakazi wa Gaza.

Ben-Gvir ameeleza kuwa, Israel imekuwa kichekesho cha Mashariki ya Kati, huku akijigamba kuwa yeye ndiye mjumbe pekee wa baraza la mawaziri la Netanyahu aliyepinga kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.
Ikumbukwe kuwa, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Nguvu za Kiyahudi (Otzma Yehudit) cha Ben-Gvir kilijiondoa kwenye serikali ya muungano ya utawala wa Kizayuni mwezi uliopita, kulalamikia makubaliano ya kusitishwa vita katika Ukanda wa Gaza.