Jihadul Islami: Hatutaruhusu kufukuzwa Wapalestina Gaza
(last modified Fri, 14 Feb 2025 12:09:37 GMT )
Feb 14, 2025 12:09 UTC
  • Jihadul Islami: Hatutaruhusu kufukuzwa Wapalestina Gaza

Mwakilishi wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina mjini Tehran amesema Wapalestina kamwe hawatakubali kutekelezwa mpango wa Marekani wa kuwaondoa kwa nguvu wakazi wa Gaza.

Katika mahojiano na IRNA, Nasser Abu Sharif amesema mpango huo, uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump, kwa hakika ni "mradi wa Kizayuni," na ambao umefuatiliwa kwa namna fulani tangu kuasisiwa kwa utawala wa Israel.

Amebainisha kuwa, kwa miaka 107, nchi za Magharibi zimekula njama chungu nzima za kuwahamisha Wapalestina kutoka katika ardhi yao na badala yake kuwaweka walowezi wa Kizayuni. Ameeleza bayana kuwa, mpango huo kwa ujumla ulishindwa huko nyuma, na utazidi kushindwa sasa na hata katika siku zijazo.

Abu Sharif amesema Wapalestina wa Ukanda wa Gaza walikataa kuondoka katika ardhi yao pamoja na kuwa jeshi la Israel liliharibu misingi yote ya riziki na kufanya mauaji makubwa ya kimbari katika kipindi cha miezi 15 katika eneo hilo lililo chini  ya mzingiro.

Ukanda wa Gaza uliyoharibiwa na mabomu ya Wazayuni

Mwakilishi wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina mjini Tehran ameongeza kuwa, mpango huo wa Rais wa Marekani utakuwa ukiukaji wa haki za binadamu na utakuwa sawa na maangamizi ya kaumu, jambo ambalo linapasa kufunguliwa mashtaka katika mahakama za kimataifa.

Mnamo Februari 4, Trump aliweka wazi nia ya nchi yake ya kuitwaa Gaza baada ya kuwafukuza Wapalestina kutoka eneo hilo na kuwahamishia katika nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Misri na Jordan.

Mpango huo wa Trump unaooana na mipango ya Wazayuni wa Israel ya kuwafukuza Wapalestina katika nchi yao, umeendelea kupingwa vikali na jamii ya kimataifa.