Kundi la Waarabu UN lapinga kufurushwa Wapalestina Gaza
Kundi la Waarabu katika Umoja wa Mataifa, pamoja na kundi la mabalozi wa Umoja wa Mataifa, wamepinga vikali mipango yoyote ya "kuwaondoa kwa nguvu" Wapalestina huko Gaza, na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Mwakilishi wa Kuwait katika Umoja wa Mataifa, Tareq Al Banai akizungumza kama mwenyekiti wa Kundi la Waarabu katika mkutano wa waandishi wa habari katika makao makuu ya UN huko New York jana Ijumaa alisema, "Kufurushwa kwa Wapalestina huko Gaza lazima kukataliwe kwa nguvu zote."
Ameeleza bayana kuwa, Kundi la Waarabu linakataa kabisa uhamishaji kama huo, ambao ni ukiukaji wa wazi wa Kifungu cha 49 cha Mkataba wa Nne wa Geneva wa 1949.
Msimamo huo wa Kundi la Waarabu UN umeungwa mkono na mabalozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).

Kadhalika Mwakilishi wa Kuwait katika Umoja wa Mataifa amelaani vitendo vya uchokozi vya utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na kuyataja mashambulizi ya utawala huo katika eneo hilo kuwa ni "ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa."
Aidha Mjumbe wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour amezungumza katika mkutano huo wa waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, "Hatuna ardhi ya asili isipokuwa Palestina. Tunaipenda Palestina, tutaujenga upya Ukanda wa Gaza. Tutaijenga upya Palestina."