HAMAS yakaribisha mpango wa Waarabu wa kuijenga upya Gaza
(last modified Thu, 06 Mar 2025 02:26:52 GMT )
Mar 06, 2025 02:26 UTC
  • HAMAS yakaribisha mpango wa Waarabu wa kuijenga upya Gaza

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imekaribisha mpango wa kuikarabati na kuijenga upya Gaza, uliopitishwa katika mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu mjini Cairo, Misri. Mpango huo pia unakusudia kuzuia kuondolewa Wapalestinakatika eneo hilo lililo chini ya mzingiro.

Hamas imesema katika taarifa yake kwamba, mkutano wa Cairo unaashiria hatua muhimu kuelekea kupatikana sauti moja ya Waarabu na Waislamu kwa kadhia ya Palestina, hasa wakati huu ambapo Israel inaendelea kushambulia na kuwahamisha watu kwenye makazi yao huko Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds.

Kundi hilo la Muqawama limewapongeza viongozi wa Kiarabu kwa kutoafiki majaribio ya kuwaondoa Wapalestina katika ardhi yao, au kudhoofisha kadhia yao ya kitaifa, na kuiita taarifa ya Cairo 'ujumbe wa kihistoria' kwamba Nakba ya pili (Janga), haitaruhusiwa.

Hamas imekaribisha wito wa kususiwa Israel kibiashara na kisiasa, ikisisitiza kuwa hiyo ndiyo "hatua ya kimkakati yenye ufanisi ya kuitenga Israel na kuishinikiza kufuata sheria za kimataifa."

Mkutano wa Waarabu uliofanyika Cairo

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas pia imehimiza udharura wa kuchukuliwa hatua zote za kivitendo za kuhakikisha kuwa mpango huo wa ujenzi wa Gaza unafanikiwa.

Jumanne, Machi 4, mji mkuu wa Misri, Cairo, ulikuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu uliolenga kujadili matukio ya hivi karibuni kuhusu suala la Palestina na kufikia uamuzi wa pamoja wa Kiarabu kuhusu Ukanda Gaza. Viongozi wa Kiarabu walioshiriki katika mkutano huo, hususan Misri na Jordan, walisisitiza uungaji mkono wao kwa mpango wa ujenzi upya wa Ukanda wa Gaza na kupinga kurejea kwa vita na uhamishaji wa Wapalestina kwa nguvu.