Arab League yalaani kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) imelaani hatua ya Israel ya kuendeleza ujenzi wa nyumba nyingine za walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina.
Arab League imeashiria uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kujenga nyumba 323 katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu na kulaani hatua hiyo. Jumuiya hiyo imesisitiza kuwa kuna ulazima kwa Israel kushinikizwa kieneo na kimataifa ili isimamishe ujenzi huo wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizoghusubiwa za Wapalestina; na kuongeza kuwa hakutakuwa na matarajio ya kuanza tena mazungumzo ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina bila ya kusimamishwa kwanza ujenzi huo wa vitongoji.
Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na huko Baitul Muqaddas Mashariki licha ya kuwa ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na vile vile umekosolewa na Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Uadilifu ya Kimataifa, lakini ungali unaendelea.