Israel yashambulia upya Gaza, yaua mamia ya Watoto na wanawake
Jeshi la utawal katili wa Israel limeua Wapalestina wasiopungua 350, ambao wengi wao ni wanawake na watoto, katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza wakati wa ukiukwaji mkubwa wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Tel Aviv na vikosi vya Muqawama vya Palestina vilivyoko Gaza.
Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti mapema Jumanne kwamba takriban watu 350 wengine pia walijeruhiwa wakati wa mauaji hayo.
Taarifa zinasema kuwa mashambulio hayo hayakuacha sehemu yoyote ya ukanda huo wa pwani ambao tayari umeathiriwa na vita na mauaji ya kimbari yaliyotokelezwa na Israel tangu Oktoba 2023.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na utawala wake 'ghasibu wa Kinazi-Kizayuni' wanabeba dhima ya mashambulio hayo ya kinyama dhidi ya raia wasio na kinga wa Gaza waliozingirwa.
Hamas imesema Netanyahu na serikali yake ya misimamo mikali wamefanya uamuzi wa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano, huku wakihatarisha maisha ya wafungwa wa Kizayuni walioko Gaza.
Hamas imetoa wito kwa wapatanishi wa kusitisha mapigano kuuwajibisha utawala wa Israel huku ikitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kusaidia Wapalestina katika "kuvunja mzingiro huo usio wa haki uliowekwa kwenye Ukanda wa Gaza." Aidha Hamas imetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa na mkutano wa dharura na kupitisha azimio linalomlazimisha Israel "kusitisha mashambulio yake."
Vita vilivyoanza tena Gaza vinakuja wakati wa hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya katika eneo hilo. Hali hiyo inatokana na uamuzi wa Netanyahu, wa kuzuia uingizaji wa misaada na bidhaa zote na kufunga vituo vya mpaka vya Ukanda huo mwishoni mwa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano.