Mpasuko Israel, Smotrich ajiondoa katika utawala wa Netanyahu
Waziri wa Fedha wa utawala haramu wa Israel, Bezalel Smotrich, ametangaza kujiuzulu kutoka wadhifa wake, jambo ambalo linaongeza matatizo ndani ya serikali ya muungano ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Televisheni cha Kanali ya 12 ya Israel iliyotolewa Jumatatu, Smotrich aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Netanyahu.
Msemaji wa Smotrich amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kupinga ombi la kinara wa chama cha mrengo mkali wa kizayuni, Nguvu Kwa Mayahudi, Itamar Ben-Gvir, ambaye alitaka nafasi zaidi za uwaziri alipotangaza kurudi katika serikali ya muungano. Ben-Gvir alikuwa amejiuzulu kutoka serikali ya Netanyahu mwezi Januari.
Smotrich sasa atarejea katika nafasi yake ya ubunge katika bunge la utawala haramu wa Israel, Knesset, kama mbunge wa chama chake cha Uzayuni wa Kidini cha mrengo mkali wa kulia.
Kujiuzulu huku hakutavunja serikali ya muungano ya Netanyahu, lakini kunaongeza mpasuko na changamoto mpya kwa serikali hiyo.
Hatua hiyo inaangazia migawanyiko inayoendelea kukua ndani ya muungano wa vyama vya siasa za mrengo wa kulia katika utawala haramu wa Israel, ambao kwa miezi ya hivi karibuni umekumbwa na mivutano kuhusu.
Ikumbukwe kuwa mwezi Januari, Ben-Gvir na chama chake kizima waliondoka katika serikali ya Netanyahu wakipinga makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.
Chama hicho kilitaja makubaliano hayo kuwa ni "kujisalimisha kwa Hamas" na kukana kile kilichoitwa mafanikio ya utawala wa Israel tangu kuanza kwa vita.
Ben-Gvir alikuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Israel pamoja na wabunge wengine wawili wa chama chake. Chama cha Nguvu Kwa Mayahudi kina viti sita kati ya 120 katika Bunge la Israel, Knesset.