Muqawama Iraq: Huenda kongozi wa Hayat Tahrir al-Sham ya Syria akamatwa akija Baghdad
(last modified Mon, 21 Apr 2025 02:25:36 GMT )
Apr 21, 2025 02:25 UTC
  • Muqawama Iraq: Huenda kongozi wa Hayat Tahrir al-Sham ya Syria akamatwa akija Baghdad

Kiongozi wa kundi la Muqawama na kupambana na ugaidi la Asa’ib Ahl al-Haq nchini Iraq ameonya kwamba, anayejiita rais wa Syria Abu Mohammed al-Jolani anaweza kukamatwa atakapowasili Baghdad, kutokana na kuwepo hati ya kukamatwa kwake.

Qais al-Khazali alitoa tahadhari hiyo katika ujumbe kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X, huku akiitaja ziara tarajiwa ya Jolani huko Baghdad kama isiyofaa na yenye matatizo kisheria.

Huku akisisitiza kuwa uhusiano thabiti kati ya Iraq na Syria ni muhimu na una maslahi kwa nchi hizo mbili, Khazali amesema muda wa sasa wa kuwa mwenyeji wa kongozi wa kundi la wanamgambo wa Hayat Tahrir al-Sham la Syria haufai.

"Kuwepo kwa rais wa sasa wa serikali ya Syria nchini Iraq ni mapema, kwani kunaweza kusababisha athari za kisheria ikiwa sheria itatekelezwa na akakamatwa na vikosi vya usalama, kutokana na kuwepo kwa hati ya kukamatwa kwake," mkuu wa Asa'ib Ahl al-Haq ameandika.

"Kwa mujibu wa kanuni ya mgawanyo wa madaraka, maamuzi ya mahakama ya Iraq lazima yafuatwe na kuheshimiwa na wote," afisa huyo wa Iraq ameongeza.

Onyo la Khazali limekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani kukutana na al-Jolani aliyejitangaza kuwa rais wa Syria huko nchini Qatar mbele ya Amir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani.