UN: Hali ya kibinadamu Gaza ni mbaya zaidi tangu vita vilipoanza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i125566-un_hali_ya_kibinadamu_gaza_ni_mbaya_zaidi_tangu_vita_vilipoanza
Msemaji wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) ameeleza wasi wasi wake mkubwa juu ya hatua ya utawala wa Israel ya kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Ukanda wa Gaza na kubainisha kwamba,  hali ya sasa ya Ukanda huo ni mbaya zaidi tangu kuanza kwa vita hivyo.
(last modified 2025-04-24T03:58:25+00:00 )
Apr 24, 2025 03:58 UTC
  • UN: Hali ya kibinadamu Gaza ni mbaya zaidi tangu vita vilipoanza

Msemaji wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) ameeleza wasi wasi wake mkubwa juu ya hatua ya utawala wa Israel ya kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Ukanda wa Gaza na kubainisha kwamba,  hali ya sasa ya Ukanda huo ni mbaya zaidi tangu kuanza kwa vita hivyo.

Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva na kueleza kwamba, Ukanda wa Gaza uko katika hali mbaya zaidi kuwahi kutokea tangu kuanza kwa vita kutokana na utawala wa Israel wa kuzuia kuingia kwa misaada ya kibinadamu.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, kuna ishara za wazi za maafa makubwa huko Gaza, na hali ya kibinadamu sasa inaweza kuwa mbaya zaidi kuliko wakati mwingine wowote wakati wa vita hivi.

Hali ya kibinadamu ya Gaza ni mbaya kiasi kwamba, hata washirika wa Israel wanajitokeza na kukosoa hatua ya Tel Aviv ya kuzuia kupelekwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Watoto wa Gaza wakisubiria chakula cha msaada.

 

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza nazo pia zimelaani hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendelea kuzuia kikamilifu misaada ya kibinadamu isiingizwe katika Ukanda wa Ghaza, na kutoa wito wa kuanzishwa mara moja utoaji misaada bila vizuizi sambamba na juhudi mpya za kusitisha mapigano.

Misaada ya kibinadamu haipaswi kamwe kutumika kama chombo cha kisiasa; na eneo la Palestina halipasi kupunguzwa au kuathiriwa na mabadiliko yoyote ya kidemografia. Israel inalazimika kwa mujibu wa sheria za kimataifa kuruhusu misaada ya kibinadamu ipitishwe bila kizuizi".