Iraq: Tunaunga mkono mazungumzo ya Iran na Marekani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq Fuad Hussein amesema kuwa, nchi yake inaunga mkono mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani.
Fuad Hussein ametangaza msimamo wa nchi yake katika mazungumzo yake mjini Baghdad na Jean-Noël Barrot, Waziri wa Mashauri wa Kigeni wa Ufaransa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq amebainisha kuwa, Baghdad ina inaunga mkono kikamilifu mazungumzo kati ya Marekani na Iran ili kuliweka kando eneo hilo na hatari ya vita. Alisisitiza kuwa "mazungumzo ndiyo suluhisho pekee, na hakuna njia mbadala za mazungumzo.
Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilifanyika Jumamosi iliyopita Aprili 12 nchini Oman huku duru ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani ikifanyika Jumamosi iliyopita Aprili 19 katika mji wa Roma nchini Italia.
Duru ya tatu ya mazungumzo ya Iran na Marekani imepangwa kufanyika Jumamosi ijayo Aprili 26.
Katika duru ya kwanza ya mazungumzo, pande mbili zilikubaliana kwamba msingi wa mazungumzo hayo utakuwa ni "Iran kufanya iaminike na itoe hakikisho kwamba programu yake ya nyuklia ni ya malengo ya amani" na mkabala wake "iondolewe vikwazo na Marekani kwa namna itakayokuwa na taathira".
Wakati huo huo, Iran imelaani vikali vikwazo vipya "haramu" ilivyowekewa na Marekani ikisisitiza kuwa vinakinzana na madai ya Washington ya kuwa na nia ya dhati ya kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu.