Mashambulio ya kinyama ya Israel yaua Wapalestina wengine 60 Ghaza, 12 wanatoka familia moja
Zaidi ya watu 60 wameuawa shahidi katika mashambulio ya kinyama ya karibuni zaidi kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza huku idadi ya vifo ikiendelea kuongezeka.
Asasi ya Ulinzi ya Raia wa Palestina na duru za tiba zimeripoti kuwa watu 12 wa familia moja kutoka Jabalia kaskazini mwa Ghaza ni miongoni mwa Wapalestina waliouawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel alfajiri ya kuamkia leo.
Wakati huohuo Wizara ya Afya ya Ghaza imetangaza kuwa hadi sasa watu 1,978 wameuawa shahidi na wengine 5,207 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni ulipovunja makubaliano ya usitishaji mapigano mnamo Machi 18, 2025.
Wapalestina wapatao 51,355 wamethibitishwa kuwa wameuawa shahidi na wengine 117,248 wamejeruhiwa katika vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza Oktoba 7, 2023.
Katika upande mwingine, Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Ghaza imetoa takwimu zake mpya za idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa na kueleza kwamba idadi hiyo imepindukia 61,700 kutokana na maelfu ya watu waliotoweka chini ya vifusi kukadiriwa kuwa wameshafariki dunia.../