Ansarullah: Hatutasitisha uungaji mkono wetu kwa watu wa Gaza
(last modified Sun, 27 Apr 2025 07:34:00 GMT )
Apr 27, 2025 07:34 UTC
  • Ansarullah: Hatutasitisha uungaji mkono wetu kwa watu wa Gaza

Naibu mkuu wa taasisi ya habari la Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza katika taarifa yake kwamba, kwa hali yoyote ile msaada na uungaji mkono wa harakati hiyo kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Gaza hautasita.

Nasruddin Amer ameeleza kuwa hakuna upande na dola lolote linaloweza kusimamisha operesheni za jeshi la Yemen katika kuiunga mkono  Gaza, na Wamarekani wameshindwa katika suala hili na wataendelea kugonga mwamba. 

Amer ameongeza kuwa: Taratibu viongozi wa Marekani wanakiri kuhusu kufeli kwao huku; na hiki ndicho tulichokieleza huko nyuma. 

Mkuu wa shirika rasmi la habari la Yemen (SABA) amesema: Uwezo wa kijeshi wa Yemen si tu kuwa haujaathiriwa na mashambulizi ya Marekani lakini pia uwezo huo, suhula na mbinu mbalimbali zimepiga hatua katika nyanja mbalimbali. 

Kuhusu uwezekano wa Marekani kuwatumia mamluki wa ndani kuyumbisha usalama wa Yemen, Nasruddin Amer amesema: " Hata katika hili tumejiandaa kwa hali zote tarajiwa, na hatuna wasiwasi katika hili."