Shambulio la 3 la kombora la hypersonic la Yemen dhidi ya Ben Gurion
(last modified Wed, 14 May 2025 11:31:50 GMT )
May 14, 2025 11:31 UTC
  • Shambulio la 3 la kombora la hypersonic la Yemen dhidi ya Ben Gurion

Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen wamefanya shambulio jipya la kombora la hypersonic dhidi ya utawala haramu wa Israel na kupelekea sauti za ving'ora vya tahadhari kuhanikiza katika sehemu ya kaskazini ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo pandikizi.

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema vikosi vyao vimevurumisha kombora la balestiki la hypersonic katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion karibu na Tel Aviv leo Jumatano, kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa Gaza, huku Wazayuni wakiendeleza mashambulizi ya umwagaji damu kwenye eneo lililozingirwa.

"Kombora hilo lilipiga shabaha yake "kwa mafanikio," na kulazimisha mamilioni ya Waisraeli kukimbilia kwenye mahandaki na kusimamisha safiri za ndege kwenye uwanja huo wa ndege kwa karibu saa moja," ameongeza.

Brigedia Jenerali Saree amesema, "Operesheni za Wanajeshi wa Yemen zinalenga kukomesha uchokozi dhidi ya watu wetu wenye msimamo na subira katika Ukanda wa Gaza, kumaliza vita vya maangamizi, na kukomesha mauaji yanayoendelea dhidi yao, machoni pa walimwengu wote." 

Hali ya mshike mshike katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion, Tel Aviv

Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimetangaza kuwa, Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion wa Israel sasa hauko salama kwa usafiri wa anga na utaendelea kuwa hivyo hadi uchokozi wa utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Gaza utakapokomeshwa na vizuizi vya misaada lilivyoekewa eneo hilo la Palestina vitakapoondolewa.

Hili ni shambulio la tatu la kombora katika muda wa chini ya saa 24 likilenga uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi na muhimu zaidi wa utawala wa Israel, wa Ben Gurion. Jeshi la Israel limethibitisha kujiri shambulio hilo la kombora, ingawaje linadai kuwa lilitungua kombora hilo la balestiki.