Jeshi la Yemen lautwanga tena kwa kombora uwanja wa ndege wa Israel
(last modified Mon, 19 May 2025 03:27:55 GMT )
May 19, 2025 03:27 UTC
  • Jeshi la Yemen lautwanga tena kwa kombora uwanja wa ndege wa Israel

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa kwa mara nyingine tena limeutwangwa kwa kombora la balestiki na droni uwanja wa ndege wa Ben Gurion wa utawala wa Kizayuni huko Tel Aviv.

Jeshi la Yemen limesema: "Kwa mara nyingine tena tumeutwangwa kwa kombora la balestiki na droni uwanja wa ndege wa Ben Gurion wa utawala wa Kizayuni huko Tel Aviv."

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree ametangaza rasmi kwamba vikosi vya Yemen ndivyo ambavyo vimeupiga kwa mara nyingine uwanja wa ndege wa Ben Gurion wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutumia kombora la balestiki na ndege isiyo na rubani.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Operesheni hizo mbili zimefanyika ikiwa ni sehemu ya kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina hasa wananchi wa Ghaza na kujibu jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu hao wasio na ulinzi. 

Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Yemen ameongeza kuwa, vipigo vya jeshi la Yemen dhidi ya maeneo nyeti na muhimu mno ya Israel vitaendelea hadi utawala wa Kizayuni utakapokomesha jinai zake huko Ghaza na kuacha kuuzingira ukanda huo. 

Majibu hayo ya jeshi la Yemen yamekuja huku taarifa zikisema kuwa, katika kipindi cha siku mbili na kidogo tu, jeshi katili la Israel limeua shahidi zaidi ya Wapalestina 200 na kuwalazimisha zaidi ya 300,000 wengine kuyakimbia makazi yao kutoka Ukanda wa Ghaza Kaskazini kuelekea kwenye Mji wa Ghaza. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Habari ya Ghaza iliyotolewa Jumamosi.