Ansarullah: Tunaendelea kushikamana na njia ya shahid Sayyid Hassan Nasrullah
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetuma pongezi kwa Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na wananchi wote wa nchi hiyo kwa mnasaba wa kukumbuka ushindi mkubwa wa Muqawama na kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon na kusisitizia wajibu wa kuendelezwa njia ya shahid wa Uislamu na ubinadamu Sayyid Hassan Nasrullah.
Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah ya Yemen jana ilitoa taarifa kwa mnasaba wa mwaka wa 25 wa kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon na kusema: Tarehe 25 Mei 2000 tulishuhudia kushindwa kwa fedheha Wazayuni na kufurushwa kusini mwa Lebanon. Ushindi wa Muqawama wa Kiislamu wa tarehe 25 Mei 2000, ulikuwa ni tukio muhimu ya kiistratijia ndani ya kalibu ya mapambano ya Waarabu na Waislamu kwa upande mmoja na adui Mzayuni kwa upande wa pili.
Taarifa hiyo imesema: "Kwa ushindi huo wa wanamapambano wa Hizbullah, wananchi wa Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu kwa mara nyingine walirejesha nguvu zao za kujiamini na mori wao wa ukombozi uliongezeka maradufu. Aidha ushindi wa Hizbullah dhidi ya adui mwaka 2006 nao ulileta mlingano mpya katika mapambano na adui."
Ansarullah Yemen pia imesema: "Tunasisitiza tena kushikamana kwetu na Hizbullah na Muqawama, na tunaendeleza njia ya viongozi waliouawa shahidi, wakiongozwa na shahidi wa Uislamu na ubinadamu, Sayyid Hassan Nasrullah, Mungu awe radhi nao.
Vile vile Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetoa mwito kwa Walebanon kupata ilhamu kutokana na mafunzo ya historia. Kwa sababu mafunzo hayo yanathibitisha kwamba nguvu ya Lebanon imo katika Muqawama wake wa kujivunia na silaha zake, silaha ambazo ndizo zinazomzuia adui Mzayuni kuvamia na kufanya inalotaka huko Lebanon.