Wabahrain waandamana tena kukosoa ukandamizaji wa Aal-Khalifa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i12685-wabahrain_waandamana_tena_kukosoa_ukandamizaji_wa_aal_khalifa
Kwa mara nyingine tena wananchi wa Bahrain katika kitongoji cha Diraz wamefanya maandaamano baada ya Swala ya Ijumaa kulaani dhulma na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 05, 2016 10:36 UTC
  • Wabahrain waandamana tena kukosoa ukandamizaji wa Aal-Khalifa

Kwa mara nyingine tena wananchi wa Bahrain katika kitongoji cha Diraz wamefanya maandaamano baada ya Swala ya Ijumaa kulaani dhulma na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.

Askari wa jeshi la utawala huo wamewazuia waumini hao kutekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Sadiq (AS) katika kijiji hicho ambacho aghalabu wa wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baada ya kila mmoja kuswali kivyake waandamanaji hao walimiminika mabarabarani katika maandamano dhidi ya utawala huo wa kifalme. Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara za kumlaani Mfamle Hamad bin Isa Al Khalifah wa nchi hiyo kwa namna anavyoiendesha nchi kwa mkono wa chuma. Aidha waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye picha za mwanachuoni mashuhuri wa Kishia nchini humo Sheikh Isa Qassim.

Maandamano ya kumuunga mkono Ayatullah Sheikh Isa Qassim

Hii ni mara ya tatu kwa watawala wa Manama kuzuia Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Sadiq katika kijiji cha Diraz.  Julai 22, maafisa usalama nchini Bahrain walizuia Swala ya Ijumaa katika msikiti huo sambamba na kuwatia mbaroni watu 50 katika kijiji hicho, kaskazini magharibi mwa nchi.

Ayatullah Sheikh Isa Qassim, mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu Bahrain

Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga kuvuliwa uraia Sheikh Isa Qassim kwa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti anachochea malumbano ya kimadhehebu na ghasia licha ya kuwa mwanachuoni huyo ni mashuhuri kwa misimamo yake ya kutetea Umoja wa Kiislamu na maandamano ya amani Bahrain.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain

Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya kupinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka uhuru, kutekelezwa uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuweko madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukijibu matakwa ya wananchi hao kwa mkono wa chuma na ukandamizaji.