Takwimu za kutisha za watoto wahanga wa njaa na vita Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129516
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema kuhusu ukubwa wa maafa ya kibinadamu huko Gaza kwamba, mamia ya watoto wamekufa kutokana na njaa na utapiamlo, na makumi ya maelfu ya wengine wamekuwa wahanga wa mashambulizi ya anga ya Israel.
(last modified 2025-08-14T09:10:13+00:00 )
Aug 14, 2025 06:43 UTC
  • Picha za kutisha kuhusu hali mbaya ya watoto Gaza
    Picha za kutisha kuhusu hali mbaya ya watoto Gaza

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema kuhusu ukubwa wa maafa ya kibinadamu huko Gaza kwamba, mamia ya watoto wamekufa kutokana na njaa na utapiamlo, na makumi ya maelfu ya wengine wamekuwa wahanga wa mashambulizi ya anga ya Israel.

Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA ameonya katika taarifa yake kwamba, hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza imefikia "kiwango kisicho na kifani" na kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za haraka kukomesha hali hii.

Lazzarini amesema katika taarifa hiyo: "Takriban watoto 100 tayari wamekufa kutokana na utapiamlo na njaa, na zaidi ya watoto 40,000 wameuawa au kujeruhiwa kutokana na milipuko ya mabomu na mashambulizi ya anga ya Israel."

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina aliongeza: "Takriban watoto 17,000 huko Gaza wanaishi bila walezi au bila familia zao, na watoto milioni moja wamepatwa na kiwewe kikubwa cha kisaikolojia na kunyimwa elimu."

Lazzarini amekosoa vikali hali hiyo ya kimataifa ya kutojali na kusema: "Hatupaswi kunyamaza pindi watoto wanapofariki dunia au kunyimwa mustakbali wao kikatili," na kusisitiza kuwa, kuendelea kwa hali hiyo kunatishia si tu kizazi cha sasa bali pia kizazi cha baadaye cha jamii nzima ya Palestina.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema: Zaidi ya watu 500,000, robo ya wakazi wa Gaza, wanakabiliwa na njaa, wakati wengine waliobaki wanakumbana na viwango tofauti vya njaa. Wameongeza kuwa watoto 320,000 walio chini ya umri wa miaka mitano wa Ukanda wa Gaza wako katika hatari ya utapiamlo mkali.