Qatar: Mpira uko katika uwanja wa Israel; Tel Aviv haitaki kufikia mapatano
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ameeleza kuwa, hivi sasa mpira uko katika uwanja wa utawala wa Kizayuni wa Israel na inaonekana kuwa Tel Aviv haitaki kufikia makubaliano ya usitishaji vita. Amesema hayo akizungumzia jibu lililotolewa na utawala wa Israel kwa pendekezo la wapatanishi.
Majid Al-Ansari amesema: "Tutaendelea kufanya na tunaunga mkono juhudi zote katika uwanja huo hadi kuhitimishwa vita katika ukanda wa Gaza.
Al Ansari amesisitiza kuwa: Israel haitaki kutoa jibu kwa mpango uliowalishwa mezani na tunaitaka jamii ya kimataifa iishinikize Tel Aviv.
Al Ansari ameongeza kusema: Mpira sasa uko katika uwanja wa Israel na utawala huo unapasa kutoa jibu kwa pendekezo lililotolewa, hata hivyo inaonekana kuwa Israel haitaki kufikia mapatano.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ameongeza kuwa: Israel imezidisha mashambulizi na hili halitakuwa na matokeo chanya.
Huku haya yakiripotiwa, maeneo mbalimbali ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu jana Jumanne yaliendelea kushuhudia maandamano ya walowezi wa Kizayuni hususan familia za mateka wa Israel wanaoshikiliwa na harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina. Huku wakichoma moto matairi na kuweka vizuizi bararani, waandamanaji wamesema kuwa wanapinga sera za baraza la mawaziri la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.