Somalia, Muqawama walaani shambulio dhidi ya Hamas nchini Qatar
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130632-somalia_muqawama_walaani_shambulio_dhidi_ya_hamas_nchini_qatar
Somalia imelaani shambulio la Israel katika mji mkuu wa Qatar, Doha ambalo liliwalenga viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, ikisema kuwa hujuma hiyo ni "ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa" na tishio kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa.
(last modified 2025-09-10T07:04:41+00:00 )
Sep 10, 2025 07:04 UTC
  • Somalia, Muqawama walaani shambulio dhidi ya Hamas nchini Qatar

Somalia imelaani shambulio la Israel katika mji mkuu wa Qatar, Doha ambalo liliwalenga viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, ikisema kuwa hujuma hiyo ni "ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa" na tishio kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake na kuchukua hatua za haraka kukomesha vitendo vya uhasama vya mara kwa mara vya Israel, sanjari na kuwadhaminia raia ulinzi na usalama wao.

Wakati huo huo, makundi ya Muqawama katika eneo la Asia Magharibi yamelaani vikali shambulio hilo la kigaidi la Israel la jana Jumanne dhidi ya viongozi wa Hamas huko Doha.

Hamas katika taarifa, imelaani jaribio la mauaji la dhidi ya ujumbe wake wa mazungumzo huko Doha. Kundi hilo la kupigania ukombozi wa Palestina limelielezea shambulio hilo kama "uhalifu wa kutisha" na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Nayo Harakati ya Muqawama wa Palestina Jihad al-Islami pia imelaani vikali kushambuliwa mkutano wa viongozi wa Hamas, na kukitaja kama "kitendo kamili cha jinai" ambacho kinapuuza viwango vya ubinadamu, maadili, pamoja na sheria na kanuni za msingi za kimataifa.

Zaidi ya hayo, Hussein al-Sheikh, Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO), amelaani shambulio hilo "baya", akisema "linaashiria ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na uhuru wa taifa la Qatar."

Nayo Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema kuwa, shambulio hilo lililowalenga viongozi wa Hamas waliokuwa wakilipitia mapendekezo ya Marekani, linathibitisha wazi kwamba utawala haramu wa Israel haupendezwi wala kufurahishwa na mazungumzo wala kutafuta suluhu.

Kwa upande wake, Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, ameyahimiza mataifa ya Kiarabu na Kiislamu "kutilia maanani" mipango miovu ya Israel kabla mambo yaharibike kabisa. "Tunaonya dhidi ya mwenendo wa kuhujumiwa nchi zote za eneo," Mashat amesema.

Hamas imethibitisha kwamba, wapatanishi wake wakuu walinusurika katika shambulio hilo, lakini wanachama watano wa kundi hilo waliuawa shahidi, akiwemo Jihad Labad, mkurugenzi wa ofisi ya afisa mwandamizi wa Hamas Khalil al-Hayya, Hammam al-Hayya, mtoto wa Khalil al-Hayya, Abdullah Abdul Wahid, Moumen Hassouna, na Ahmed al-Mamloukan ambao wametajwa kama washiriki wa mkutano huo.