UNIFIL yaitaka Israel ikomeshe mashambulizi, iondoke kikamilifu katika ardhi ya Lebanon
Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon, UNIFIL imesema, shambulio la anga lililofanywa na jeshi la Israel jana usiku kusini mwa Lebanon ni ukiukaji wa wazi wa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama na tishio la moja kwa moja kwa hali tete ya uthabiti katika eneo hilo.
Taarifa iliyotolewa na UNIFIL imesema, kufuatia shambulio hilo, "walinda amani katika ngome mbili za Deir Kifa, karibu na Burj Qalawieh, walikimbilia maeneo ya hifadhi kwa ajili ya usalama. Mashambulizi hayo yaliweka maisha ya wanajeshi wa Lebanon, walinda amani wa Umoja wa Mataifa na raia katika hatari. Tunatoa wito kwa Israel [wanajeshi] kujiepusha na mashambulizi yoyote zaidi na kujiondoa kikamilifu katika eneo la Lebanon".
Ndege za kivita za jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel zimefanya mashambulizi ya anga ya mtawalia katika maeneo ya kusini mwa Lebanon, ukiwa ni ukiukaji wa karibuni zaidi wa makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyofikiwa kati ya utawala huo na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon ya Hizbullah na ambayo yalisainiwa Novemba 2024.
Jeshi la Lebanon limelaani kuendelea ukiukaji wa sheria unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel, ambazo umeripotiwa kuwa umeshapindukia mara 4,500 tangu yalipotekelezwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo imesema, mashambulizi ya Israel yalivilenga vijiji vya kusini na maeneo mengine yenye wakazi, na kusababisha vifo vya raia na kupingana na madai ya utawala huol kwamba mashambulizi hayo yalilenga ngome za Hizbullah.../