Hamas yaitaka jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuitenga Israel
Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, imekaribisha hatua ya kutambuliwa kwa taifa la Palestina na mataifa ya Uingereza, Australia na Kanada, ikieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuthibitisha haki ya Wapalestina juu ya ardhi yao.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, harakati hiyo imeitaka jumuiya ya kimataifa pamoja na Umoja wa Mataifa kuutenga utawala wa Israel na kusitisha aina zote za ushirikiano na utawala huo wa kibeberu.
Hamas imesifu hatua ya kutambuliwa taifa la Palestina kuwa ni mafanikio makubwa katika kuthibitisha haki ya Wapalestina juu ya ardhi na maeneo yao matakatifu, sambamba na ndoto ya kuanzishwa kwa taifa huru lenye mji mkuu wake Al-Quds (Jerusalem).
Harakati hiyo imeeleza kuwa kutambuliwa huko ni “matokeo yanayostahili kutokana na jitihada, ustahimilivu na kujitolea kwa watu wetu” katika harakati zao za ukombozi na kurejea katika ardhi yao.
Hamas imesisitiza kuwa kutambuliwa kwa Palestina kunapaswa kuambatana na hatua za vitendo, ikiwemo kusitishwa mara moja kwa “vita ya kikatili vya mauaji ya kimbari” katika Ukanda wa Gaza, pamoja na juhudi za kupinga mipango ya utekaji na Uyahudishaji katika Ukingo wa Magharibi na Al-Quds.
Harakati hiyo pia imetoa wito wa kuongezwa vikwazo dhidi ya Israel na watawala wake pia wawajibishwe kutokana na jinai dhidi ya ubinadamu.
Taarifa hiyo imekosoa vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuendelea kupuuza sheria za kimataifa na kanuni za kibinadamu, ikibainisha “ukiukaji wa kutisha” dhidi ya watu wa Palestina.
Tamko hili limetolewa wakati ambapo kuna mabadiliko makubwa ya kidiplomasia kuhusu kutambuliwa kwa Palestina katika jukwaa la kimataifa.
Matangazo kutoka kwa mataifa makubwa ya Magharibi na washirika wa muda mrefu wa Israel yanaashiria kuongezeka kwa hali ya kutengwa kwa utawala wa Israel kimataifa, hasa kutokana na vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Kutambuliwa kwa Palestina ni hatua ya kinembo inaonesha kuongezeka kwa uungwaji mkono wa kimataifa kwa taifa la Palestina na haki yake ya kujitawala.
Hata hivyo, wakosoaji wanasema kuwa hatua kama hizi kutoka kwa mataifa yanayoiunga mkono Israel kifedha na kijeshi ni mbinu ya kuendeleza uungwaji mkono wao kwa Tel Aviv huku wakionekana kuambatana na maoni ya umma wa kimataifa.