Wananchi Bahrain waendeleza maandamano dhidi ya serikali
Wananchi wa Bahrain kwa mara nyingine tena wamekusanyika mbele ya nyumba ya kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo Ayatullah Sheikh Issa Qassim mapema leo kuonyesha uungaji mkono wao kwa mwanachuoni huyo wa Kiislamu.
Kadhalika wananchi hao wa Bahrain wamefanya maandamano katika maeneo mbali mbali ya nchi hususan katika kijiji cha Diraz, kuulani utawala wa Aal-Khalifa kwa kumvua uraia msomi na mwanaharakati huyo wa kidini.
Aidha maandamano kama hayo yalishuhudiwa jana usiku katika eneo la al-Bilad al-Qadeem, viungani mwa mji mkuu Manama, kisiwa cha Sitra na kitongoji cha Sar, kusini mwa mji mkuu huo. Licha ya maandamano ya amani, vyombo vya usalama vya Bahrain vimekuwa vikiwakandamiza waandamanaji na wapinzani wa utawala huo.
Kituo cha Haki za Binadamu nchini Bahrain kimekosoa vikali ukandamizaji na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na utawala wa Aal Khalifa. Mkuu wa Jukwaa Kwa Ajili ya Haki za Binadamu nchini Bahrain (BFHR) amesema kuwa, utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa ungali unaendelea kufanya ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu.
Baraza la Maulamaa wa Bahrain linasema mashitaka anayolimbikiziwa Ayatullah Qassim ambaye utawala wa Manama umemvua uraia, ni ya kubuni na wala hayana mashiko na kwamba kesi dhidi yake inakiuka katiba, haki za binadamu zilizoanishwa katika sheria za nchi hiyo na hata za kimataifa.
Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya kupinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka uhuru, kutekelezwa uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuweko madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukijibu matakwa ya wananchi hao kwa mkono wa chuma na ukandamizaji mkubwa.