Baghdad yairuhusu Russia kutumia anga yake dhidi ya Daesh
Baghdad imesema kuwa Russia imeruhusiwa kwa masharti kutumia anga ya Iraq kuendesha mashambulizi dhidi ya kundi la Daesh huko Syria.
Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq amesema hivi na hapa ninamnukuu," tumewafungulia anga zetu Warusia. Hatujapokea ombi lolote rasmi kutoka Russia kuhusu kupitishwa aina yoyote ya makombora katika anga zetu." Mwisho wa kunukuu. Waziri Mkuu wa Iraq aliyasema hayo Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari huko Baghdad.
Amesema ndege za Russia zitakuwa zikitumia maeneo yaliyotengwa ya mpakani kuendeshea mashambulizi yao na kwamba ndege hizo hazitakuwa zikiruka katika miji ya Iraq. Waziri Mkuu wa Iraq ameongeza kuwa ameziruhusu ndege za kivita za Russia kutumia anga ya Iraq kwa sababu amepokea taarifa ya wazi kuhusu ndege hizo. Amesema ndege hizo zinaendesha mashambulizi kwa uangalifu na kujiepusha na kusababisha vifo vya raia.

Russia imekuwa ikiendesha mashambulizi dhidi ya Daesh na makundi mengine ya kigaidi na kitakfiri huko Syria tangu Septemba 30 mwaka jana kufuatia ombi la Rais wa nchi hiyo Bashar al Assad.