Wayemen waandamana kupinga kuvunjiwa heshima Qur'an Marekani
-
Wayemen waandamana kupinga kuvunjiwa heshima Qur'an Marekani
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen walimiminika katika barabara na mitaa ya Sa’ada jana Ijumaa kushiriki maandamano ya kulaani kitendo cha kunajisiwa Qur'ani Tukufu nchini Marekani, sanjari na kupaza sauti zao kuiunga mkono Palestina, huku hasira zikiongezeka katika ulimwengu wa Kiislamu kutokana na wimbi la vitendo vya hivi karibuni vilivyo dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Maandamano hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu, "uhamasishaji wa jumla na utayari wa kuunga mkono Qurani takatifu na Palestina," kulingana na Al-Masirah ya Yemen. Mikutano kama hiyo pia imefanyika katika miji mingine kadhaa ya Yemen katika siku mbili zilizopita.
Hii ni baada ya Jake Lang, mgombea wa mrengo mkali wa chama tawala cha Republican katika uchaguzi wa Seneti ya Marekani, kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu wakati wa maandamano ya kupinga Uislamu yaliyofanyika Jumapili iliyopita huko Plano, Florida.
Washiriki wa maandamano nchini Yemen walinyanyua nakala za Qurani na mabango yanayoonyesha msimamo usioyumba kuelekea kitabu kitakatifu cha Uislamu. Waandamanaji hao wamesisitiza kwamba, "tusi lolote kwa Qurani Tukufu linamaanisha shambulio kwa Ummah mzima [wa Kiislamu]."
Kitendo hicho cha kichochezi kimezua hasira na ghadhabu kutoka kwa Waislamu na wanaharakati wa haki za binadamu, na kutazamwa kama uchokozi wa wazi na dharau kwa hisia za mabilioni ya Waislamu duniani kote.
Jumanne iliyopita, Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah nchini Yemen alilaani vikali kitendo hicho cha kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu kilichofanywa na mwanasiasa wa Marekani huku akiwataka Waislamu kote duniani kusimama imara kulinda matukufu yao.
Kabla ya hapo, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani kwa maneno makali uhalifu na kitendo kiovu kilichofanywa na Mmarekani cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu, ikielezea tukio hilo kuwa la kichochezi linalotoa harufu mbaya ya chuki, na shambulio la wazi dhidi ya matakatifu zaidi ya Waislamu na maadili ya kidini na ya kibinadamu yanayowakilishwa na dini zote za mbinguni.