Wapiganaji wa Hizbullah wakabiliana na jeshi vamizi la Israel kusini mwa Lebanon
Wapiganaji wa harakati ya mapambano ya Hizbullah wamekabiliana na vikosi vya Israel vilipokuwa vikijaribu kupenya katika maeneo ya kusini mwa Lebanon, wakilenga mikusanyiko ya wanajeshi na magari ya kijeshi kwa mashambulizi ya makombora pamoja na droni za kujitoa mhanga.
Katika taarifa kadhaa zilizotolewa Jumapili, Hizbullah ilieleza kuwa wapiganaji wake waligundua msafara wa kijeshi wa Israel uliokuwa umeingia katika mji wa kusini wa Majdal Zoun, ulioko katika wilaya ya Tyre (Sour). Wapiganaji wa muqawama kisha walitekeleza shambulizi la kuvizia, wakitumia silaha nyepesi na za kati pamoja na makombora ya kurushwa begani (RPG) katika operesheni iliyodumu kwa takribani saa mbili.
Hizbullah ilisisitiza kuwa magari kadhaa ya kijeshi ya Israel yaliyokuwa yakiandamana na kikosi hicho yaliharibiwa na kuteketea kwa moto wakati wa makabiliano. Wakati huohuo, wapiganaji wa muqawama wa Lebanon walivurumisha makombora yaliyolenga mikusanyiko ya wanajeshi wa Israel katika maeneo ya kusini na kusini-mashariki mwa Majdal Zoun.
Operesheni hizi za karibuni zinajiri wakati vikosi vya Israel vimeongeza juhudi za kujiimarisha katika maeneo ya miinuko kote kusini mwa Lebanon, hususan katika maeneo yanayozunguka Nabatieh na Tyre.
Uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Lebanon unaambatana na ripoti za juhudi za kidiplomasia zilizozidi kushika kasi kuhusu uwezekano wa hati ya maelewano kati ya Iran na Marekani, huku mazungumzo yakiripotiwa kuzingatia utekelezaji wa usitishaji vita nchini Lebanon na mustakabali wa uwepo wa vikosi vya kigeni katika eneo hilo.
Tangu Machi 2, Israel imekuwa ikiendesha operesheni ya kijeshi dhidi ya Lebanon, hali iliyopelekea vifo vya zaidi ya watu 3,700 na kujeruhi zaidi ya 11,480, sambamba na kuwafanya zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao.
Hata baada ya kutangazwa kwa usitishaji vita tarehe 17 Aprili, Tel Aviv imeendelea na mashambulizi, ikihusika katika mashambulizi ya kila siku ya mizinga na uharibifu mkubwa wa makazi katika vijiji vingi.