Misri yafunga tena kivuko cha Rafah
Misri imefunga tena kivuko cha Rafah, njia pekee inayotumiwa kufikishia misaada ya dharura kwa Wapalestina walio chini ya mzingiro huko Ghaza.
Wizara ya Ndani ya Harakati ya Hamas huko Ghaza imetoa taarifa na kusema wakuu wa Misri wamefunga kivuko cha Rafah baada ya kukifungua kwa muda wa siku tatu tu.
Taarifa hiyo imesema wakaazi wa Ghaza wapatao 2,439 kutoka Ghaza walitumia fursa hiyo kuondoka eneo hilo huku wengine 1,122 wakiingia.
Ghaza imekuwa chini ya mzingiro wa kinyama wa Israel kwa muda wa karibu miaka kumi sasa ambapo Wapalestina wamekuwa wakitumia fursa ya kufunguliwa kivuko hicho kutekeleza shughuli za dharura.
Idadi kubwa ya Wapalestina wanaoishi Ghaza husoma katika vyuo vikuu ya Misri huku wengine wakitembelea familia zao katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Hamas imesema katika mwaka 2015, kivuko cha Rafah kilifunguliwa kwa muda wa siku 21 tu na hivyo kuufanya mwaka huo kuwa mbaya zaidi kwa watu wa Ghaza. Hali ya Wapalestina wa Ghaza imekuwa mbaya zaidi baada ya jeshi kumtimua madarakani rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, Mohammad Morsi mnamo Julai 2013. Mtawala wa sasa wa Misri, Abdel Fattah el Sisi, ambaye alikuwa mkuu wa jeshi wakati wa kupinduliwa Morsi, amekuwa akishirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwakandamiza Wapalestina huko Ghaza.