Jeshi la Yemen laangamiza makumi ya mamluki wa Saudia mkoani Ta'izz
-
Msemaji wa jeshi la Yemen, Yahya Saree
Msemaji wa Vikosi vya Jeshi la Yemen amesema vitengo vya kijeshi vya nchi hiyo vimeendesha operesheni kubwa dhidi ya vibaraka wa Saudia katika mkoa wa kusini-magharibi wa Ta’izz, na kuwaua na kuwajeruhi makumi yao.
Brigedia Jenerali Yahya Saree ametangaza katika taarifa kuwa wanajeshi wa Yemen wamewalenga wapiganaji wanaofadhiliwa na Saudi na maghala yao ya silaha katika mji wa bandari wa Mokha kwenye pwani ya Bahari Nyekundu siku ya Jumapili, kwa kutumia makombora ya masafa marefu na ndege droni za kujitoa mhanga.
Ameongeza kuwa makombora hayo na ndege zisizo na rubani ziliifikia kwa usahihi shabaha zilizolengwa, na kusababisha hasara kubwa kwa wakala hao wanaoungwa mkono na Saudi.
Jenerali Saree alibainisha kuwa operesheni hiyo kubwa ilifanyika wakati wakala hao walipokuwa wakifanya mkusanyiko mkubwa wa kijeshi na kujiandaa kushambulia vikosi vya Yemen.
Afisa huyo mkuu wa kijeshi wa Yemen amesisitiza kuwa mashambulizi yanayoendelea ya mamluki wa Saudia kwenye pwani ya magharibi ya Yemen, na hasa katika mkoa wa Ta’izz, yanalenga kuizuia taifa la Yemen lisikabiliane na mzingiro usio wa haki wa Saudi na uvamizi wa kikatili, ambao umeendelea kwa karibu miaka 12.
Jenerali Saree amesema: “Hatutamruhusu adui Msaudi afanikishe malengo yake ya kuwashambulia watu wetu, na kuwaingiza watoto wetu katika handaki la mauti ili kutumikia ajenda yake ya fitina kwa niaba ya maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.”
Ameongeza kuwa: “Vikosi vya Jeshi la Yemen, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, vitaendelea kufuatilia kwa karibu harakati zote na mikusanyiko ya mamluki wa Saudia, na vitawalenga kwa usahihi na moja kwa moja. Watu wetu wa Yemen na vikosi vyetu vya jeshi vitaendelea na kaulimbiu ya ‘mzingiro kwa mzingiro’, na vitashambulia mikusanyiko yoyote ya kijeshi inayolenga raia wa Yemen na maeneo yaliyokombolewa.”
Tarehe 20 Julai, serikali ya Yemen ilitangaza mzingiro wa baharini dhidi ya Saudi Arabia, ikisema mamlaka za Riyadh zimeiwekea Yemen “mzingiro usio wa haki na wa kinyama” kwa karibu miaka 12, “zikipora rasilimali zetu na kuweka mzingiro kamili.”
Baadaye, Vikosi vya Jeshi la Yemen vimeripoti operesheni nyingi zilizofanikiwa dhidi ya meli zinazohusishwa na Saudi Arabia katika Bahari Nyekundu.
Tangu Machi 2015, Saudi Arabia na washirika wake wameweka mzingiro dhidi ya Yemen, wakianzisha vita vya kina vilivyopewa msaada wa kijeshi, kisiasa na kilojistiki na Marekani pamoja na baadhi ya nchi za Magharibi. Vita hivyo vimewaua makumi ya maelfu ya Wayemeni, lakini Saudi Arabia imeshindwa kufanikisha lengo lake kuu la kurudisha utawala wa kibaraka nchini humo.