Safari ya kutia shaka ya ujumbe wa Marekani nchini Iraq
Kanali ya televisheni ya al-Ittijah ya Iraq imeripoti habari ya safari ya ujumbe wa Marekani mjini Baghdad siku chache tu baada ya kuarifishwa balozi mpya wa nchi hiyo huko Iraq.
Ofisi ya Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq sanjari na kutoa ripoti juu ya suala hilo imetangaza kuwa timu ya Marekani inayoundwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi katika kongresi ya Marekani ilikutana jioni ya Jumamosi na kufanya mazungumzo na waziri mkuu huyo mjini Baghdad. Katika kikao hicho pande mbili zilijadili juu ya utayarifu wa kijeshi kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa genge la kigaidi la Daesh. Kwa mujibu wa kanali ya al-Ittijah, katika kikao hicho kulijadiliwa pia suala la kutolewa mafunzo na kudhamini mahitaji ya silaha kwa jeshi la Iraq. Baada ya Stuart Jones kumaliza muda wake wa kuhudumu kama balozi nchini Iraq, Douglas Silliman ameteuliwa kurithi mikoba ya afisa huyo wa Marekani. Jumamosi ya wiki iliyopita, Ibrahim al-Jaafari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq alikutana na Stuart Jones ambapo pande mbili zilisisitizia udharura wa ushirikiano wa nchi zote za dunia katika kupambana na ugaidi, huku Washington ikitolewa mwito wa kuwa jadi katika suala hilo. Safari ya ujumbe wa Marekani nchjini Iraq imetajwa na pande tofauti nchini humo kuwa yenye kutia shaka hususan katika wakati huu ambapo kunaandaliwa operesheni kabambe kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Hii ni kusema kuwa, harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq inayoitwa Hashdu al-Shabi, imekuwa na nafasi chanya katika operesheni hizo. Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo, harakati hiyo imekuwa na nafasi muhimu sana katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi nchini humo. Tajriba ya mafanikio ya Hashdu al-Shabi ilishuhudiwa katika vita vyake na genge la Daesh katika operesheni za kuukomboa mji wa Fallujah na maeneo mengine ya Iraq, ambapo ilithibitika uwezo mkubwa wa wapiganaji wa harakati hiyo ya wananchi. Uzoefu chanya wa harakati hiyo katika operesheni za kuukomboa mji wa Mosul ni muhimu na jambo linalotakiwa a waanchi wa Iraq lakini baadhi ya mirengo ya kisiasa na maadui wa Iraq wanafanya njama za kufelisha mafanikio ya kuusafisha mji huo wa Mosul kutokanan na wanachama wa genge hilo. Marekani ni moja ya nchi zinazopinga kutumika mafanikiona uzoefu wa Hashdu al-Shabi na kwa kushirikiana na Saudia, imekuwa ikiitaja harakati hiyo kuwa ni harakati iliyopitwa na wakati na isiyofaa. Kuituhumu harakati hiyo muhimu nchini Iraq kunajiri katika hali ambayo Washington na Riaydh zinazodai kupambana na ugaidi zilihusika katika kutoa himaya kwa wanachama wa genge la Daesh (ISIS) mjini Mosul na kufanikisha kuanguka mji huo mikononi mwa genge hilo. Siasa za Marekani baada ya kuvamiwa kijeshi Iraq hapo mwaka 2003, hazikuwa kwa maslahi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Hii ni kusema kuwa, baada ya uvamizi huo, kulizaliwa kundi hilo la kigaidi chini ya himaya kamili ya Marekani sanjari na kutekeleza njama katika kuibua mpasuko baina ya makundi ya kisiasa nchini Iraq, huku baadaye kukiundwa muungano bandia wa kile kinachodaiwa kuwa ni wa kupambana na Daesh, muungano unaoongozwa na Washington yenyewe. Miamala hiyo inabainisha uhasama wa siasa za Marekani dhidi ya Iraq, na hata Ibrahim al-Jaafari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq baada ya kumalizika muda wa balozi wa Marekani, ameitaka Marekani kushirikiana kwa dhati na Baghdad katika vita dhidi ya ugaidi. Ukweli ni kwamba, nafasi ya Marekani katika vita vyake eti vya kupambana na Daesh kupitia muungano uliotajwa, haijakuwa na faida yoyote ghairi ya kuharibu miundombinu ya taifa hilo. Mashambulizi ya anga ya ndege zisizokuwa na rubani za Marekani yamekuwa yakikosea shabaha ambapo badala ya kushambulia maeneo ya magaidi, yamekuwa yakilenga raia na kusababisha hasara kubwa za roho na mali. Kama tulivyosema nafasi ya kisiasa na kijeshi ya Marekani dhidi ya Iraq tangu kujiri mashambulizi ya mwaka 2003 hadi leo hayajakuwa na maslahi yoyote kwa serikali ya baghdad .