Iran: Jumuiya ya Kiarabu iseme ukweli na isiufumbie macho
(last modified Sat, 10 Sep 2016 04:11:40 GMT )
Sep 10, 2016 04:11 UTC
  • Iran: Jumuiya ya Kiarabu iseme ukweli na isiufumbie macho

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taarifa ya hivi karibuni ya Baraza la Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Kiarabu dhidi ya Iran haina ukweli na kimsingi inautumikia utawala wa Saudi Arabia.

Bahram Qassemi akitoa radiamali yake kwa taarifa hiyo ya mawaziri wa Arab League amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaliusia baraza hilo liwe ni lenye kufikiria vizuri, liseme ukweli na lisiifumbia macho haki.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, uungaji mkono wa upande mmoja na uliojaa taasubi wa viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa baadhi ya nchi wanachama katika miaka ya hivi karibuni si tu haujasaidia chochote katika kuyapatia ufumbuzi matatizo na migogoro ya Mashariki ya Kati, bali umepelekea kuvurugika zaidi hali ya usalama na amani katika eneo hili  na kuzidi kuupa kiburi utawala wa Riyadh cha kuendelea kuua wananchi wasio na hatia wa baadhi ya nchi za Kiarabu.

Kikao cha Arab League

Bahram Qassemi amesemakwamba, kama kweli Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wana nia ya dhati ya kusaidia mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati kuishi kwa amani na usalama na kama wana nia ya kweli ya kuimarisha ujirani mwema, basi waitake Saudia iache kufanya ukandamizaji na mauaji dhidi ya wananchi wa Syria, Iraq, Yemen na Bahrain na iache pia kuyaunga mkono makundi ya kigaidi.

Kuhuasiana na faili na maafa ya Mina, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, matarajio ya familia  za mashahidi wa tukio hilo la mwaka jana katika ibada ya Hija ni kufahamika ukweli na wakati huo huo utawala wa Saudia kutoa majibu ya kueleweka kuhusiana na maafa ya Mina.